Waziri Mkuu wa Malaysia: Amani ya dunia inategemea amani ya Palestina
Waziri Mkuu wa Malaysia, Mahathir Mohammed amesema iwapo dunia inataka kushuhudiwa amani endelevu, sharti kadhia ya Palestina ipatiwe ufumbuzi.
Dakta Mahathir Mohammed aliyasema hayo katika dhifa ya futari aliyoiandaa Jumatano jioni alipompokea Mkuu wa Zamani wa Tawi la Kisiasa la Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Palestina (HAMAS), Khalid Mash'al huko Putrajaya, mji mkuu wa kisiasa wa Malaysia.
Amesema, "Sababu kuu ya kuchipuka ugaidi katika eneo la Asia Magharibi ni kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina na utawala ghasibu wa Israel, sambamba na mashambulizi mtawalia dhidi ya Wapalestina katika ardhi zao zilizoghusubiwa."
Waziri Mkuu wa Malaysia amebainisha kuwa, ugaidi na misimamo mikali ni matunda ya ugaidi wa kiserikali wa Israel, huku akiitaka jamii ya kimataifa itekeleze wajibu wake wa kuushurutisha utawala wa Kizayuni uondoke katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu, na kuruhusu wakimbizi wa Kipalestina kurejea katika ardhi zao za jadi.
Kadhalika amekosoa vikali sera za utawala haramu wa Israel za kutaka kufuta utambulisho wa Quds Tukufu huku akilaani mashambulizi ya Wazayuni dhidi ya Waislamu Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Zamani wa Tawi la Kisiasa la Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Palestina (HAMAS) amemtaja Dakta Mahathir Mohammed kama kiongozi shupavu wa ulimwengu wa Kiislamu, huku akiutaja mpango wa Marekani wa 'Muamala wa Karne" kuwa njama za kutaka kuhitimisha muqawama wa Wapalaestina dhidi ya ukaliaji wa mabavu wa ardhi zao unaofanywa na Tel Aviv.
Huku akipongeza msimamo wa Malaysia wa kuwaunga mkono Wapalestina na kuupiga vita utawala wa Kizayuni, Khalid Mash'al amesema sera kuu ya utawala haramu wa Israel ni kuuyahudisha mji mtukufu wa Quds unaokaliwa kwa mabavu, na kuendelea kuwafanyia ukatili Wapalestina wa Gaza.