Zarif akutana na Waziri Mkuu wa Pakistan mjini Islamabad
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran yuko safarini nchini Pakistan, ambapo amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo mjini Islamabad.
Katika kikao hicho cha Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif, pande mbili zimejadili juu ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili pamoja na masuala ya kieneo na kimataifa.
Wawili hao wamegusia kuhusu njia na mikakati inayopaswa kufanywa kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa Tehran na Islamabad katika nyuga tofauti hususan katika sekta ya nishati na miundombinu.
Kabla ya kukutana na Imran Khan, Dakta Zarif alikutana na kufanya mazungumzo na mwenzake wa Pakistan Shah Mehmood Qureshi na Mkuu wa Majeshi ya nchi hiyo Jenerali Qamar Javed Bajwa.
Baada ya kuwasili mjini Islamabad jana, Zarif alisema atawasilisha pendekezo la Tehran kwa serikali ya Islamabad la kuunganishwa bandari ya Gwadar ya Pakistan na bandari ya Chabahar iliyoko kusini mashariki mwa Iran, ili kuimarisha mabadilishano ya kibiashara baina ya nchi mbili hizi.
Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Aprili, Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa nchi yake, alifanya safari nchini Iran na kukutana na viongozi wa nchi hii, ambapo alisisitiza kuwa, Tehran na Islamabad zinaweza kutoa mchango mkubwa katika kuleta utulivu na amani katika nchi za eneo la Asia Magharibi ikiwemo Afghanistan.
Aidha Tehran na Islamabad zilikubaliana kuunda kikosi cha pamoja cha radiamali ya haraka cha kupambana na ugaidi katika mpaka wao wa pamoja.