Romania yasema haina mpango wa kuuhamishia ubalozi wake Quds
Katibu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Romania amesema nchi hiyo ya Ulaya haina mpango wowote wa kuuhamishia ubalozi wake mjini Quds huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, kutoka Tel Aviv.
Maria Magdalena Grigore amesema hayo katika mkutano wake na Ayman Safadi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan mjini Amman na kuongeza kuwa, nchi yake itaendelea kufungamana na 'msimamo wake wa kihistoria'.
Waziri huyo wa Romania kadhalika amepongeza nafasi chanya ya Jordan katika kuimarisha usalama na uthabiti katika eneo la Asia Magharibi, huku akisisitiza kuwa mkutano wake na mwenzake huyo wa Jordan umekuwa wa kufana.
Itakumbukwa kuwa, Mei mwaka jana Rais Klaus Lohannis wa Romania alikosoa vikali na kutaja kama uvumi kauli ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Viorica Dancila aliyedai kwamba nchi hiyo imefikia uamuzi wa kuhamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv, kwenda mji wa Quds (Jerusalem).
Rais huyo wa Romania alisisitiza kuwa: "Hatuwezi kufuata siasa za kigeni ambazo zinaenda kinyume na sheria za kimataifa."
Inafaa kuashiria kuwa, baadhi ya nchi zimefuata kibubusa sera za Washington na kuafiki suala la kuhamisha balozi zao kutoka Tel Aviv kwenda mji wa Quds (Jerusalem), kitendo ambacho kinakiuka sheria za kimataifa.
Itakumbukwa kuwa tarehe 6 Disemba mwaka jana Rais Donald Trump wa Marekani aliutangaza mji huo wa Quds (Jerusalem) kuwa mji mkuu wa utawala khabithi wa Israel, na miezi michache baadaye akauhamisha ubalozi wa nchi yake kutoka Tel Aviv kwenda mji huo.