Misri: Rais Tayyip Erdoğan ana uhusiano na kundi la Ikhwanul Muslimin
Serikali ya Misri kupitia Waziri wake wa Mambo ya Nje imemtuhumu Rais Tayyip Erdoğan wa Uturuki kuwa ana uhusiano na kundi la Ikhwanul Muslimin.
Sameh Shoukry, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri aliyasema hayo Alkhamisi kufuatia matamshi ya Rais Erdoğan aliyoyatoa kuhusiana na kifo cha Mohamed Morsi, Rais wa zamani wa Misri na kusema kuwa, matamshi hayo sio ya kuwajibika. Aidha Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amesema kuwa, Rais Tayyip Erdoğan anataka kufunika masuala ya ndani ya nchi yake kwa kuingilia masuala ya nchi nyingine na kwamba Cairo itakabiliana na kila aina ya vitisho dhidi yake. Sameh Shoukry ameongeza kwamba matamshi ya rais huyo wa Uturuki yanabainisha kuwa ana uhusiano na kundi la Ikhwanul Muslimin. Itakumbukwa kuwa, serikali ya Misri ililitangaza kundi la Ikhwanul Muslimin kuwa la kigaidi sambamba na kulipiga marufuku nchini humo.
Jumanne iliyopita Rais Tayyip Erdoğan wa Uturuki akitoa radiamali kufuatia kifo cha rais wa zamani wa Misri, Mohamed Morsi alisema kuwa kifo hicho hakikuwa cha kawaida. Rais huyo wa zamani wa Misri aliaga dunia siku ya Jumatatu iliyopita akiwa mahakamani akisikiliza kesi yake inayohusiana na faili la tuhuma za ujasusi. Uhusiano wa Uturuki na Misri uliharibika miaka ya hivi karibuni baada ya jeshi la Misri kufanya mapinduzi dhidi ya Mohamed Morsi, chini ya usimamizi wa Jenerali Abdel Fattah el-Sisi, rais wa sasa wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.