Jeshi la Iran liko tayari kumfanya mvamizi alipe gharama kubwa
Kamanda mwandamizi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema vikosi vya jeshi la Iran havitaki vita lakini daima viko imara kulihami na kulilinda taifa lao kwa gharama yoyote ile.
Meja Jenerali Gholam Ali Rashid, Kamanda wa kikosi cha Khatam al-Anbiya amesema hayo leo Jumatatu alipotembelea vituo vya kijeshi vya Iran karibu na Lango Bahari la Hormoz na kusisitiza kuwa, "Tunaonya kuwa, iwapo vita vitaibuka, hakuna yeyote akakayeweza kuvidhibiti na kutasawari ukubwa wake."
Amesisitiza kuwa maadui hawana uwezo wala uthubutu wa kuishambulia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwamba jeshi la Iran liko tayari kumfanya mvamizi alipe gharama kubwa kwa chokochoko zake.
Ameeleza bayana kwamba, usalama wa taifa na kulinda mipaka ya ardhini, baharini na angani ya nchi ni vipaumbele vikuu vya vikosi vya ulinzi vya Iran na kwamba leo hii Jamhuri ya Kiislamu inajitosheleza kwa vifaa vya ulinzi ikiwemo mifumo ya kujilinda kwa makombora.
Kauli ya kamanda huyo wa kikosi cha Khatam al-Anbiya cha (IRGC) inajiri siku chache baada ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuitungua ndege isiyo na rubani ya RQ-4 Global Hawk ambayo ni miongoni mwa ndege za kisasa kabisa za ujasusi za Marekani na inayogharimu dola milioni 220, baada ya kuingia katika anga ya Iran kinyume cha sheria.
Marekani haijaweza kutoa ushahidi wowote wa maana kuthibitisha madai yake kuwa eti droni hiyo ilitunguliwa katika anga ya kimataifa. Badala yake Rais Donald Trump alitangaza vikwazo vipya vya kiuchumi dhidi ya taifa hili, kama jibu kwa pigo hilo la kijeshi.