Maduro akosoa hatua za Trump dhidi ya Venezuela
(last modified Tue, 20 Aug 2019 02:33:53 GMT )
Aug 20, 2019 02:33 UTC
  • Maduro akosoa hatua za Trump dhidi ya Venezuela

Kufuatia kuendelea vitisho na mashinikizo ya Marekani dhidi ya Venezuela, Rais Nicolas Maduro wa nchi hiyo amekosoa hatua za Rais Donald Trump dhidi ya nchi yake na kusema: "Hatua ambazo Rais wa Marekani anachukua dhidi ya Venezuela ni sawa na zile ambazo kiongozi wa Wanazi alichukua katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia."

Maduro ameashiria hatua za Marekani kuzuia Venezuela kuuza nje bidhaa zake na pia kuagiza bidhaa kutoka nje. Halikadhalika amesema Marekani imefunga akaunti za benki za Venezuela mbali na kuwawekea vikwazo viongozi wengi wa nchi hiyo, akiwemo makamu wa rais Delcy Rodríguez kwa tuhuma  bandia za kuhusika na biashara ya mihadarati. Maduro amesisitiza kuwa, biashara ya kimataifa ya dawa za kulevya inaendeshwa na Marekani na kuongeza kuwa, wakati Delcy Rodríguez alipokuwa waziri wa mambo ya ndani wa Venezuela kuanzia mwaka 2008 hadi 2012, alitoa pigo kubwa kwa wafanya biashara wa kimatiafa wa dawa za kulevya. Ikumbukwe kuwa biashara haramu ya dawa za kulevya kimataifa ni moja ya vyanzo vikuu vya pato kwa uchumi wa Marekani.

Katika miaka ya hivi  Marekani imekuwa ikitekeleza njama kadhaa dhidi ya Venezuela ikiwa ni pamoja na kuwaunga mkono wapinzani, kuunga mkono mapinduzi ya kijeshi na kutoa vitisho vya mashambulizi ya kijeshi, lengo kuu likiwa ni kuiangusha serikali halali ya Venezuela.

Rais Trump wa Marekani

Lakini Marekani imefeli katika katika njama zake zote hizo na hivyo viongozi wa Washington hivi sasa wameshadidisha vikwazo vya kiuchumi na mashinikizo ya kisiasa kwa lengo la kuilazimisha serikali ya Venezuela isalimu amri na hatimaye kuiangusha serikali ya Maduro. Katika miezi ya hivi karibuni, Marekani imewaweka viongozi wengi wa Venezuela katika orodha ya vikwazo. Halikadhalika vikwazo vya mafuta, fedha na benki vingali vinaendelea.

Hatua hizo za viongozi wa Marekani zimesababisha matatizo makubwa kwa uchumi wa Venezuela.

Ripoti kuhusu hali ya uchumi wa Venezeula zinaonyesha kuwa, vikwazo vimepelekea nchi hiyo kukumbwa na uhaba wa dawa, chakula na umeme na hivyo kuyafanya maisha ya wananchi kuwa magumu.

Imedokezwa kuwa zaidi ya Wavenezuela 40,000 wamefariki dunia katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kutokana na athari za vikwazo vya Marekani ambavyo vinakiuka sheria.

Aidha kwa mujibu wa takwimu, vikwazo hivyo vya Marekani vimeisababishia Venezuela hasara ya zaidi ya dola bilioni 100.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela Jorge Arreaza anasema hivi kuhusu vikwazo hivyo: "Vikwazo vya Marekani havimuathiri tu Maduro na serikali bali vimeiathiri nchi nzima."

Viongozi wa Marekani wanataka kuiwekea Venezuela mashinikizo ya juu ili hatimaye Rais Nicolas Maduro aondoke madarakani lengo kuu likuwa ni kupora utajiri wa nchi hiyo na kuidhibiti kisiasa.

Ni kwa msingi huo ndio wiki iliyopita Rais Trump akatoa amri ya kufungwa akaunti zote za Venezuela na kuzuia mali zote za nchi hiyo huko Marekani sambamba na kutisha kuyawekea vikwazo mashirika yote ya mafuta ambayo yanafunga mikataba na Venezuela.

Kuendelea uhasama huo wa Marekani kumepelekea Maduro asimamishe mazungumzo baina ya wawakilishi wa serikali na wapinzani. Hivi sasa viongozi wa Venezuela wanatekeleza mkakati maalumu wa kisiasa na kiuchumi ili kukabiliana na mashinikizo ya Marekani.

Maduro amesema, uhasama wa Marekani una lengo la kuiangusha serikali ya Venezuela na kuyafanya maisha ya wananchi kuwa magumu lakini amesisitiza kuwa nchi yake iko tayari kusimama kidete na hatimaye kusambaratisha njama za Marekani.

Kinara wa upinzani  Venezuela Juan Guaido 

Hivi sasa kwa mara nyingine Maduro amesisitiza kuwa, Venezuela iko tayari kukabiliana na sera za Kihitler za Trump katika vita hivyo vya kiuchumi na kisiasa visivyo na mlingano.

Inaelekea kuwa, pamoja na kushadidi mashinikizo ya Marekani dhidi ya Venezuela, Maduro bado ana uungaji mkono wa wananchi; na jeshi na kwa kutegemea nguzo hizo mbili ataweza kutatua matatizo yatokanayo na uhasama wa Washington.

Tags