Mwito wa Uingereza wa kukomeshwa ukiritimba wa sarafu ya dola
(last modified Mon, 26 Aug 2019 01:38:12 GMT )
Aug 26, 2019 01:38 UTC
  • Mwito wa Uingereza wa kukomeshwa ukiritimba wa sarafu ya dola

Msimamo wa Marekani wa kutumia vibaya sarafu ya dola katika masuala ya biashara na ya fedha kimataifa kwa lengo la kufanikishia malengo yake haramu, umewakasirisha hata waitifaki wa karibu mno wa Washington kama vile Uingereza ambayo sasa imetoa mwito wa kukomeshwa ukiritimba wa matumizi ya sarafu ya dola duniani.

Mwito huo kama tulivyosema haukutolewa na wapinzani wa kimataifa wa Washington, kama vile Russia na China, bali umetolewa na muitifaki wa karibu mno wa Marekani yaani Uingereza.

Mark Carney, Gavana wa Benki Kuu ya Uingereza amesema kuwa, kuna udharura kwa Benki Kuu za dunia kuungana ili kuendesha mapambano ya kubadilisha mfumo wa hivi sasa wa akiba za fedha za kigeni. Amesema: Ukiritimba wa sarafu ya dola katika mfumo wa fedha duniani umepelekea kuongezeka madhara na hasara kwa nchi za dunia kutokana na kuweko riba ya kiwango cha chini na ustawi dhaifu wa Marekani. Kwa mtazamo wa Gavana wa Benki Kuu ya Uingereza, karibuni hivi sarafu ya Yuan ya China itaipiku sarafu ya dola ya Marekani na kushika nafasi ya kwanza kimatumizi duniani hivyo dola si sarafu ya kuaminika tena. 

Mark Carney

 

Gavana huyo wa Benki Kuu ya Uingereza amesema kuwa, tatizo la mfumo wa fedha duniani hivi sasa ni kupambana na siasa za utakatishaji fedha. Matamshi hayo ya Mark Carney yalikuwa yanaashiria siasa za kibiashara na kiuchumi za rais wa Marekani, Donald Trump ambaye ameamua kuzusha mizozo na kudanganya walimwengu pamoja na kuanzisha vita vya kibiashara na dunia nzima zikiwemo China na Ulaya kwa lengo la kuuletea matatizo mfumo wa fedha na biashara duniani. Siasa za rais wa Marekani za kujikumbizia kila kitu upande wake na kutumia mabavu dhidi ya mataifa mengine hasa kuwawekea vikwazo wapinzani na maadui wa Marekani na kufikia hadi ya kutishia kuwawekea vikwazo hata marafiki na waitifaki wa karibuni wa Marekani, zimezifanya nchi nyingi duniani hata washirika wa Marekani barani Ulaya kuamua kupambana na Washington na kuilaumu White House kwa kutumia vibaya sarafu ya dola kujinufaisha binafsi na kuzishinikiza nchi nyingine. Siasa za Marekani za kutoa vitisho na kuzishinikiza nchi nyingine kwa kutumia sarafu ya dola na mabadilishano ya fedha, zimepelekea kuzuka wimbi la mwamko wa kimataifa wa kupunguza kutegemea sarafu ya dola na kutumia sarafu nyingine katika mabadilishano ya kibiashara, jambo ambalo ni kwa madhara ya sarafu ya dola ya Marekani. Mwamko huo bila ya shaka utapunguza sana ushawishi wa dola ya Kimarekani katika mabadilishano ya kifedha na kibiashara ulimwenguni. 

Ni kwa sababu hiyo ndio maana Gavana wa Benki Kuu ya Uingereza akasema kuwa kinachofanywa na sarafu ya dola hivi sasa ni kuvuruga mfumo wa fedha duniani. Vile vile ametoa mwito kwa nchi za dunia kuanzisha mfumo wa kambi kadhaa utakaoundwa na sarafu zenye thamani duniani ili kukomesha ukiritimba wa sarafu ya dola. Gavana wa Benki Kuu ya Uingereza amekwenda mbali zaidi na kufikia hata kupendekeza kuanzishwa mfumo maalumu wa fedha za kigeni wa kidijitali na kutiwa nguvu vyanzo vya kifedha vya Mfuko wa Kimataifa wa Fedha, IMF. Kwa kweli hatua ya kiongozi wa ngazi za juu wa fedha wa Uingereza ya kuwa na mtazamo kama huo kuhusu nafasi hasi na ovu ya sarafu ya dola ni ushahidi kuwa licha ya kwamba London na Washington zina umoja wa kiistratijia baina yao, lakini siasa za Donald Trump ni mbovu kiasi kwamba madhara yake hayakumbakisha yeyote, bali yameifikia hata Uingereza ambayo ni muitifaki wa karibu mno wa Marekani.

Rais Donald Trump wa Marekani

 

Leo hii nchi nyingi duniani zimeamua kupunguza utegemezi wao kwa sarafu ya dola katika mabadilishano yao ya kifedha na ndio maana nchi nyingi zikiwemo hata za marafiki wa Marekani zimeamua kuchukua hatua maalumu za kupunguza matumizi ya dola katika miamala yao ya kigeni. Jambo hilo limepunguza hisa ya sarafu ya dola katika akiba za kimataifa za fedha na kuongezeka hisa ya sarafu nyinginezo kama vile Euro. Victoria Crwomberg, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: Umoja wa Mataifa umezitaka nchi za dunia kufanya juhudi za kuanzisha sarafu mpya ya fedha ya kutumiwa na umoja huo kwa ajili ya akiba ya kimataifa kutokana na hatari za kiuchumi zinazotokana na kuyumba thamani ya dola ambayo hivi sasa inatumiwa na Umoja wa Mataifa kama sarafu pekee ya akiba yake. 

Kwa kweli Marekani inatumia vibaya udhaifu wa mashirika, mabenki na mifumo ya fedha ya kimataifa wa kutegemea dola katika miamala yao. White House inatumia sarafu ya dola kama fimbo ya kuzilazimisha nchi za dunia kutii amri zake au kuacha kufuata siasa zisizopendwa na Washington. Hata hivyo, siasa hizo ghalati za Marekani zimepelekea kuzuka mwamko wa kupambana vilivyo na ukiritimba wa sarafu ya dola, jambo ambalo ni kwa madhara ya uchumi wa Marekani.