Waziri Mkuu wa Pakistan: Njia ya mashahidi wa Karbala, lazima iendelezwe
(last modified Wed, 11 Sep 2019 12:08:43 GMT )
Sep 11, 2019 12:08 UTC
  • Waziri Mkuu wa Pakistan: Njia ya mashahidi wa Karbala, lazima iendelezwe

Waziri Mkuu wa Pakistan, Imran Khan sambamba na kuashiria kumalizika kwa marasimu ya kidini ya kumi la kwanza la mwezi wa Muharram nchini Pakistan, amesema kuwa raia wa nchi hiyo hususan Waislamu wa jimbo la Kashmir, ni lazima waendeleze ujumbe wa mashahidi wa Karbala.

Imran Khan ameitaja siku ya Ashura kwa anwani ya vita dhidi ya udikteta na dhulma na kuongeza kuwa, mashahidi wa Karbala walionyesha kwamba, mapambano dhidi ya udikteta yatapata ushindi. Inafaa kuashiria kuwa, jana Waislamu wa madhehebu ya Shia na wapenzi wa Ahlul-Bayti wa Mtume (saw) nchini Pakistan walihuisha katika maeneo tofauti ya nchi hiyo marasimu ya kumbukumbu za siku ya Ashura ya Imam Hussein (as), mjukuu wa Mtume Muhammad, kwa kukumbuka kuuawa shahidi mtukufu huyo pamoja na wafuasi wake waaminifu.

Maombolezo ya Siku ya Ashura katika nchi za Afrika

Katika kumbukumbu hizo, Waziri Mkuu wa Pakistan alisisitiza kuwa: "Karbala ni mapambano na kusimama imara dhidi ya dhulma. Kwa ajili hiyo ni lazima uhakika huu na ujumbe wake viendelee kubakia hai." Waziri Mkuu wa Pakistan aliongeza kwamba, kama walivyotuonyesha mashahidi watukufu wa Karbala, mapambano dhidi ya udikteta ni lazima yatapata ushindi. Marasimu ya kumbukumbu za Ashura, yaliendelea hadi jioni ya Jumanne ya jana nchini Pakistan. Mbali na Pakistan, marasimu ya kumbukumbu za tukio hilo chungu la Ashura, yalifanyika katika nchi mbalimbali za dunia, ambapo wapenzi wa Ahlul-Bayti wa Mtume walighiriki katika maombolezo ya Imam Hussein (as), mjukuu wa mtukufu huyo (saw).

Tags