Aug 21, 2024 11:53 UTC
  • Mazuwari 28 raia wa Pakistan waaga dunia katika ajali ya basi Iran

Raia 28 wa Pakistan wamepoteza maisha huku makumi ya wengine wakijeruhiwa baada ya basi lililokuwa limewabeba kubingiria katika kaunti ya Taft, mkoani Yazd, katikati ya Iran. Mazuwari hao walikuwa wakielekea katika mji mtakatifu wa Karbala nchini Iraq kwa ajili ya kushiriki Arubaini ya Imam Hussein AS.

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kudhibiti Dharura mkoani Yazd, Mohammad Ali Malekzadeh ameliambia shirika la habari la IRNA kuwa, watu 23 wamejeruhiwa kwenye ajali hiyo, na kwamba 14 miongoni mwao wapo katika hali mahututi.

Amesema majeruhi wamelazwa katika hospitali ya Abarkuh katika kaunti ya Taft, na kwamba abiria sita miongoni mwa waliojeruhiwa wametibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Habari zaidi zinasema kuwa, ajali hiyo ilitokea mwendao wa saa nne usiku wa kuamkia leo Jumatano. Imeelezwa kuwa, ajali hiyo ilihusisha basi lililokuwa likisafirisha abiria 51, wote wakiwa raia wa Pakistan waliokuwa wakisafiri kwenda Iraq kwa ajili ya Arubaini ya Imam Hussein AS.

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kudhibiti Dharura mkoani Yazd ameongeza kuwa, mamlaka za eneo hilo kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, zinapanga kusafirisha miili na majeruhi wa ajali hiyo kwa ndege hadi Pakistan.

Mazuwari kutoka maeneo mbalimbali ndani ya Iraq na maeneo mengine ya dunia wameendelea kumiminika katika mji wa Karbala kwa ajili ya kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Hussein (as).

Mji wa Karbala umeanza kushuhudia wimbi kubwa la umati wa watu wanaoingia mjini humo wengine wakitembea kwa miguu kutoka miji mbalimbali kama ya Basra na Najaf kuelekea mjini humo.

Tags