Juncker asisitiza kudhibitiwa mipaka iwapo Brexit itafikiwa bila ya mapatano
Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya amesisitiza kuhusu kudhibitiwa mipaka iwapo Uingereza itajitoa Umoja wa Ulaya bila ya kufikia mapatano.
Jean Claude Juncker amesema kuwa Brussels itasimamia mipaka ya Ireland ili kulinda maslahi ya Umoja wa Ulaya iwapo kutatekelezwa Brexit pasina na mapatano. Amesema aidha Brussels itabuni mpaka mpya kati ya Jamhuri ya Ireland na Ireland ya kaskazini. Juncker amesisitiza kuwa Umoja wa Ulaya hauhusiki kivyovyote na athari za kujitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya bila ya mapatano na ni Uingereza yenyewe ndio itakayokuwa imesababisha athari hizo.
Kuhusu suala la kusimamia mpaka wa Ireland, Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya amesema kuwa, mpango huo unalenga kulinda haki za masoko ya ndani na ya Ireland. Hii ni katika hali ambayo, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ametaka kufutwa kwa mpango huo wa kusimamiwa mpaka wa Ireland.
Johson anasisitiza kwamba hadi kufikia Oktoba 31 mwaka huu Uingereza lazima itoke Umoja wa Ulaya iwe kwa kufikia mapatano au la. Pamoja na hayo, bunge la Uingereza limepasisha mswada kwa lengo la kuzuia kutekelezwa Brexit bila ya mapatano na wakati huo huo kumlazimisha Waziri Mkuu wa nchi hiyo kufanya juhudi za kuakhirishwa kujitoa nchi hiyo EU; ambapo kwa mujibu wake, Johnson anapasa kuuomba Umoja wa Ulaya urefushe uanachama wa London ndani ya EU kwa miezi mitatu mingine.