Taliban yataka kutekelezwa vipengee vya makubaliano ya Qatar
(last modified Sat, 19 Oct 2019 05:40:47 GMT )
Oct 19, 2019 05:40 UTC
  • Taliban yataka kutekelezwa vipengee vya makubaliano ya Qatar

Msemaji wa Idara ya Siasa ya kundi la Talibal la Afghanistan amesema kuwa Marekani inakwamisha utekelezwaji wa makubaliano ya Qatar.

Suheil Shaheen amejibu matamshi yaliyotolewa na katibu Mkuu wa shirika la kijeshi la nchi za Magharibu NATO akisema: Makubaliano ya Marekani na Taliban yaliyofikiwa baada ya mazungumzo ya muda mrefu kuhusu suala la kuondoka wanajeshi wa kigeni huko Afghanistan yako wazi, na Marekani inapaswa kuondoa majeshi yake katika ardhi ya Afghanistan.

Katika kikao cha hivi karibuni cha viongozi wa NATO, Katibu Mkuu wa shirika hilo, Jens Stoltenberg alitoa wito wa kupewa dhamana na kundi la Taliban kwa ajili ya kutekeleza makubaliano hayo.

Suhail Shaheen ameashiria vipengee vya makubaliano hayo kama ulazima wa kuondoka askari wa kigeni nchini Afghanistan, kutotumia ardhi ya nchi hiyo dhidi ya Marekani na washirika wake na kupunguza mivutano na machafuko na kusema, watu wasiotaka makubaliano hayo ni wapinzani wa mazungumzo ya amani nchini Afghanistan.

Wawakilisi wa Marekani na Taliban katika mazunhumzo ya Qatar

Matamshi ya msemaji wa Idara ya Siasa ya Taliban nchini Qatar kwamba Marekani inakwamisha utekelezaji wa makubaliano ya pande mbili yanaonesha kwamba, kuna mwafaka kuhusiana na suala la kuzitisha vita. Japokuwa hii ni mara ya kwanza upande mmoja wa makubaliano ya amani ya Afghanistan huko Qatar kutoa habari ya kuwepo mapatano ya kusitisha vita yaliyofikiwa baina ya wawakilishi wa Taliban na mjumbe maalumu wa Marekani Zalmay Khalilzad huko Qatar, lakini nukta muhimu zaidi katika matamshi ya Suhail Shaheen ni kwamba, mapatano hayo yalikuwa ya awali na hayakuweza kusainiwa kutokana na Donald Trump kufuta mazungumzo ya pande hizo mbili. 

Swali linalojitokeza hapa ni kwamba, ni kwa nini msemaji wa Idara ya Siasa ya Taliban akatangaza waziwazi suala la mapatano ya hayo baada ya kupita karibu miezi miwili tangu Trump afute na kusitisha mazungumzo ya pande mbili? 

Inaonekana kuwa, matamshi ya Katibu Mkuu wa shirika la NATO yanayotaka kuchukuliwa dhamana kutoka kwa kundi la Taliban kwa ajili ya utekelezaji wa mapatano yoyote tarajiwa ndiyo sababu ya kufichuliwa na kutangazwa waziwazi habari ya mapatano ya kundi hilo na Marekani kuhusiana na kusimamisha mapigano huko Afghanistan. Hasa ikitiliwa maanani kwamba, wakati wote wa mazungumzo ya Taliban na Marekani yaliyoendelea kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja na baada ya mazungumzo hayo kutupiliwa mbali na Donald Trump, Washington daima imekuwa ikitumia mbinu ya kulituhumu kundi hilo kwamba halilegezi misimamo na kwamba halina nia ya kukomesha vita nchini Afghanistan.

Mazunumzo ya amani Aghanistan yamekwama baada ya Trump kuyatupilia mbali

Salman Rafii Sheikh ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: "Vita vya miaka 18 vilivyoanza kwa mashambulizi ya Marekani dhidi ya Afghanistan bado vinaendelea na Washington imeshindwa kufikia malengo ya uvamizi wake dhid ya nchi hiyo. White House ndio kikwazo kikuu cha kupatikana amani katika nchi hiyo."

Matamshi ya Suhai Shaheen aliyesema kuwa Marekani inakwamisha mwenendo wa utekelezaji wa makubaliano ya amani nchini Afghanistan ni jibu kwa misimamo ya White House ambayo daima inafungamanisha suala la kutokoma na kusita vita huko Afghanistan na msimamo ya kundi la Taliban. Matamshi hayo yameonesha kuwa, Marekani ndiyo inayokwamisha mchakato wa kurejeshwa amani katika nchi hiyo kwa kuzuia kundoka majeshi ya kigeni katika ardhi ya Afghanistan.

Tags