Uturuki yamrejesha mwanachama wa ISIS nchini Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i57200-uturuki_yamrejesha_mwanachama_wa_isis_nchini_marekani
Uturuki imesema imemrejesha mwanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) katika nchi yake ya Marekani, huku Ankara ikianza kuwarejesha makwao magaidi wa genge hilo la ukufurishaji iliowakamata.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 11, 2019 07:54 UTC
  • Uturuki yamrejesha mwanachama wa ISIS nchini Marekani

Uturuki imesema imemrejesha mwanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) katika nchi yake ya Marekani, huku Ankara ikianza kuwarejesha makwao magaidi wa genge hilo la ukufurishaji iliowakamata.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uturuki, Ismail Catakli amesema nchi hiyo itaanza kuwarejesha makwao wanachama hao wa ISIS kuanzia leo Jumatatu. Ameongeza kuwa, wanachama saba wa ISIS raia wa Ujerumani watarejeshwa katika nchi yao mnamo Novemba 14.

Naye Suleyman Soylu, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki ameeleza bayana kuwa, "Uturuki sio hoteli ya kuwahifadhi wanamgambo wa ISIS, Ankara itaanza leo shughuli ya kuwarejesha wapiganaji hao katika nchi zao."

Serikali ya Ankara hata hivyo haijataja idadi kamili ya wanachama hao wa Daesh walioko nchini humo au nchi watakakopelekwa.

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki

Uturuki katika wiki za hivi karibuni imekuwa ikizikosoa nchi za Ulaya kwa kukataa kuwapokea raia wao waliojiunga na ISIS katika nchi za Iraq na Syria, na kusisitiza kuwa itawarejesha kwa nguvu katika nchi hizo hata kama wamevuliwa uraia.

Haya yanajiri siku chache baada ya Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki kutoa vitisho tena kwamba nchi yake itawafungulia milango mamilioni ya wakimbizi wa Syria waliopo Uturuki kuelekea nchi za bara Ulaya, iwapo nchi za Umoja wa Ulaya hazitotoa msaada kwa serikali ya Ankara kuhusiana na wakimbizi wa Syria waliopo nchini kwake.