Nov 26, 2019 04:39 UTC
  • Watu wenye chuki watishia kulipua  kwa bomu msikiti mjini Berlin, Ujerumani

Viongozi wa msikiti wa Sehitlik mjini Berlin, mji mkuu wa Ujerumani wametangaza kwamba watu wenye chuki dhidi ya dini ya Uislamu miongoni mwa makundi ya mrengo wa kulia na yenye misimamo ya kigaidi, wametishia kulipua kwa bomu msikiti huo.

Taarifa iliyotolewa na viongozi wa msikiti huo imesema kuwa mapema Jumatatu ya jana walipata ujumbe wa barua pepe kutoka kwa kundi la mrengo wa kulia na lenye misimamo mikali ya kigaidi ambapo lilidai kwamba limetega mada za miripuko ndani ya msikiti huo. Msikiti huo ambao unamimilikiwa na taasisi ya Waislamu wa Uturuki, ni eneo mashuhuri la kufanyia ibada kwa ajili ya Waislamu wa mjini Berlin. Katika miezi ya hivi karibuni makumi ya misikiti ndani ya Ujerumani imekumbwa na vitisho vya kutegwa mada za miripuko ndani yake suala ambalo limeitia wasi wasi mkubwa jamii ya Waislamu wa nchi hiyo ya Ulaya.

Waislamu nchini Ujerumani wanaopitia wakati mgumu kutokana na kubaguliwa

Aidha katika miaka ya hivi karibuni Ujerumani imeshuhudia ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu linalotokana na propaganda chafu na hatua za vyama vyenye misimamo mikali ya kigaidi vya mrengo wa kulia. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwaka 2018 zaidi ya misikiti 100 pamoja na asasi mbalimbali za kidini nchini Ujerumani zilishambuliwa huku polisi ya nchi hiyo ikisajili zaidi ya kesi 813 za mashambulizi dhidi ya Waislamu.

Tags