Russia yapinga kuwa Iran pekee ndio itekeleze ahadi za JCPOA
(last modified Sun, 01 Dec 2019 12:06:50 GMT )
Dec 01, 2019 12:06 UTC
  • Russia yapinga kuwa Iran pekee ndio itekeleze ahadi za JCPOA

Kwa kuzingatia juhudi zinazofanywa na wanachama wa nchi za Magharibi katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA za kutaka kutekeleza matakwa haramu ya Marekani ya kuitaka Iran kuwa ndio pekee iwe daima inafungamana na mapatano hayo ya nyuklia, serikali ya Russia imepinga wazi takwa hilo na kulitaja kuwa jambo lisilowezekana.

Mikhail Ulyanov, mwakilishi wa Russia katika taasisi za Umoja wa Mataifa zenye makao yake mjini Vienna amezungumzia takwa la nchi za Ulaya la kutaka vipengee vyote vya JCPOA vilivyo na uwezekano wa kupunguzwa, kufanywa kuwa vya kudumu na kusema: "Kwa mtazamo wa sheria za kimataifa, madhumuni ya vipengee vinavyoweza kupunguzwa katika mapatano ya JCPOA ni uamuzi wa hiari wa Iran kwa ajili ya kupunguza kwa muda baadhi ya haki zake chini ya mkataba NPT." Madhumuni ya 'vipengee vyenye uwezekano wa kupunguzwa' katika mapatano hayo ambavyo pia vinajulikana kwa jina la 'vipengee vya machweo' ni vipengee katika mapatano ya nyuklia ambavyo utekelezaji wake hukoma baada ya kupita kipindi fulani. Kwa msingi huo, Marekani na baadhi ya wakosoaji wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA, wanaamini kuwa suala la Iran kuhitimishiwa baadhi ya vifungu hivyo katika miaka ijayo ni nukta za kasoro za mapatano hayo, hivyo wanaitaka Tehran iendelee kutekeleza vifungu hivyo daima.

Mikhail Ulyanov, mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa mjini Vienna

Kuhusiana na suala hilo Abbas Araghchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amezungumzia 'vifungu vya machweo' katika mapatano ya JCPOA na kusema: "Ukweli ni kwamba msingi wa mapatano, yaani kufungamana Iran na kutozalisha silaha za maangamizi, ni jambo la kudumu na Iran imeahidi kwamba haitoelekea upande huo." Amezidi kubainisha kwamba: "Sababu ya miradi ya nyuklia ya Iran yenye malengo ya amani kuwekewa baadhi ya mipaka na vizuizi vya hadi miaka 10, 15 na sehemu nyingine miaka 20 na 25, ni kujenga hali ya kuaminiana, na bila shaka hakuna nchi yoyote inayoweza kutarajiwa kuendelea kujenga uaminifu huo milele." Itakumbukwa kuwa tarehe 8 Mei mwaka huu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa ni mwaka mmoja tangu Marekani ijiondoe kwa upande mmoja katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na baada ya nchi za Ulaya kushindwa kutekeleza kivitendo majukumu yake ya kufidia hasara za kiuchumi zilizotokana na kujiondoa huko, Tehran iliamua kupunguza na kusimamisha baadhi ya majukumu yake katika mapatano hayo. Hii leo pia ukiwa umepita zaidi ya mwezi mmoja tangu nchi hii ilipoanza kutekeleza hatua yake ya nne ya kupunguza majukumu yake ndani ya JCPOA, wanachama wa mapatano hayo miongoni mwa nchi za Ulaya ambazo ni Uingereza, Ufaransa na Ujerumani wamepandwa na hasira kiasi cha kuwafanya viongozi wa serikali ya Paris kutoa vitisho vya kurejesha vikwazo dhidi ya Iran. Hii ni katika hali ambayo nchi za Ulaya wanachama wa mapatano hayo ya nyuklia, zilikuwa zimeahidi kudhamini maslahi ya Iran kupitia mfumo maalumu wa mabadilishano ya kifedha wa (INSTEX). Hata kama nchi hizo zilibuni mfumo huo na kuahidi kuutekeleza kivitendo, lakini zimeshindwa kutekeleza ahadi zao kutokana na mashinikizo ya Marekani.

Nchi zilizosalia katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA

Hivi sasa pia katika hatua nyingine mpya ya kipropaganda nchi sita zingine za Ulaya, zimetangaza kujiunga na mfumo huo wa INSTEX. Nchi hizo ambazo ni Ubelgiji, Denmark, Sweden, Finland, Norway na Uholanzi, zimetoa taarifa ya pamoja juu ya umuhimu wa kulindwa na kutekelezwa kikamilifu mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kuongeza kuwa, zipo katika mchakato wa kujiunga na mfumo huo maalumu wa kifedha. Aidha nchi hizo zimeitaka Iran kufungamana kikamilifu na vipengee vya mapatano hayo haraka iwezekanavyo. Ombi hilo limetolewa ambapo hadi sasa nchi za Ulaya za kundi la 4+1 hazijachukua hatua yoyote ya maana kwa ajili ya kuyalinda mapatano hayo ya nyuklia, hususan katika kufunguliwa mfumo huo wa INSTEX. Inaonekana kwamba kwa sasa mapatano ya JCPOA yamefika katika nukta nyeti. Baada ya kumalizika muda wa subira yake ya kistratijia, Iran imeanza kutekeleza hatua yake ya nne ya kupunguza majukumu yake katika mapatano hayo kama ambavyo viongozi wa Tehran wametangaza kuwa iwapo nchi wanachama wa Ulaya hazitochukua hatua ya kivitendo kwa ajili ya kuyanusuru mapatano hayo, kamwe haitolazimika kufungamana nayo. Hii ni katika hali ambayo baada ya Marekani kujiondoa kwenye mapatano tajwa, si tu kwamba nchi za kundi la 4+1 zimeshindwa kuchukua hatua yoyote ya kivitendo, bali zimeendelea kuwa na matarajio yasiyo ya kimantiki kwa kuitaka Tehran pekee iendelee kutekeleza majukumu yake na ifungamane milele na ahadi zake. Kama alivyosema Mikhail Ulyanov, mwakilishi wa Russia katika taasisi za Umoja wa Mataifamjini Vienna: "Mbali na kwamba Marekani imejiondoka kwenye mapatano ya JCPOA, imezizuia pia nchi nyingine kuipatia Iran kile ambacho inastahiki kukipata huku ikiitaka ifungamane na vifungu vyote vya mapatano hayo, suala ambalo kimsingi ni lenye mgongano wa wazi."

Tags