Dec 05, 2019 07:13 UTC
  • Kuendelea mashinikizo ya Marekani dhidi ya Venezuela; kuwekewa Caracas vikwazo vipya

Serikali ya Marekani imeendeleza mashinikizo yake dhidi ya Venezuela ambapo imeiwekea nchi hiyo vikwazo vipya katika sekta ya viwanda na biashara ya mafuta.

Jumanne ya juzi ya tarehe 3 Disemba, Wizara ya Hazina ya Marekani ilitangaza kuziweka katika orodha yake ya vikwazo meli sita za mafuta zilizokuwa na jukumu la kusafirisha mafuta ya Venezuela kuelekea Cuba. Justin Muzinich, Naibu Waziri wa Hazina wa Marekani amesema kuhusiana na vikwazo hivyo kwamba: Havana na Caracas zimebadilisha majina ya meli za kubeba mafuta na kurahisisha kuchukua mafuta kutoka Venezuela kwenda Cuba na hivyo kufanya juhudi za kukwepa vikwazo.

Vikwazo hivyo vipya vinatangazwa katika hali ambayo, ni kwa muda sasa ambapo Marekani imekuwa ikifanya kila iwezalo ili iwe na satua na ushawishi katika nchi za Amerika ya Latini hususan katika nchi kama Venezuela na Cuba ambazo zikishikamana na sera za kupigania uadilifu na kupinga ukoloni zimesimama kidete dhidi ya Marekani. Venezuela ikiwa moja ya nchi muhimu zaidi katika eneo la Amerika ya Latini kwa muda mrefu sasa imekuwa ikiandamwa na njama za kila namna za Marekani hasa kutokana nchi hiyo kuwa na utajiri mkubwa wa nishati ya mafuta.

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela

Kuanzia Januari mwaka huu, serikali ya Marekani ilianza kutekeleza siasa na mikakati mbalimbali kama ya vikwanzo dhidi ya Venezuela na kuwaunga mkono wapinzani hususan Juan Guaido, kiongozi wa upinzani nchini humo ambaye alijitangaza kuwa Rais.

Hatua ya Marekani ya kuunga mkono mapinduzi na kutishia kuishambulia kijeshi Venezuela ni upande mwingine wa njama za Washington za kutaka kuiondoa madarakani serikali halali ya mrengo wa kushoto nchini humo inayoongozwa na Nicolas Maduro na kisha kuiweka madarakani serikali ambayo itakuwa tiifu na itakayodhamini maslahi ya Washington katika nchi hiyo.

Jorge Arreaza, Waziri wa Mashauri ya Kigenin wa Venezuela amesema kuwa: Marekani ambayo inafanya kila iwezalo ili iwe na satua kwa siasa na vyanzo vya utajiri vya Venezuela, imeanzisha vita vya kila upande dhidi ya nchi hiyo, ili iweze kuwa na udhibiti wa maliasili na siasa za nchi hiyo. Vita hivyo vya kila upande dhidi ya Venezuela ambavyo vinasimamiwa na kuongozwa na mashirika ya kiintelijensia ya Marekani, lengo lake ni kuiondoa madarakani serikali halali ya Rais Nicolas Maduro.

Juan Guaido, kiongozi wa upinzani nchini Venezuela

Licha ya kuwa, mpaka sasa njama na mashinikizo ya Marekani dhidi ya Venezuela yamegonga mwamba, lakini viongozi wa Washington hawajakata tamaa na filihali wamo mbioni kutumia wenzo wa vikwazo dhidi ya serikali ya Caracas na hivyo kuubana uga wa Maduro na hivyo kuandaa mazingira ya kuisambaratisha serikali yake. Katika uga huo, Cuba nayo ikiwa mshirika wa Venezuela inalengwa na vikwazo vya Marekani kiasi kwamba, juma lililopita Shirika la Cuba la Panamericana liliwekewa vikwazo kutokana na kufanya shughuli zake katika sekta ya mafuta ya Venezuela.

Rais Miguel Diaz-Canel wa Cuba sanjari na kulaani siasa za chuki na uadui za Marekani dhidi ya nchi zenye siasa za mrengo wa kushoto za Amerika ya Latini amesisitiza kwamba: Marekani ingali imejizatiti na kukusanya nguvu  zake kwa ajili ya kupora maliasili na utajiri wa nchi za mrengo wa kushoto za Amerika ya Latini. Marekani imekuwa ikichukua kila hatua dhidi ya Venezuela na kwa mara nyingine tena imekuwa ikikariri uvamizi wake wa kijinai dhidi ya Cuba katika nchi nyingine. Miongoni mwa uvamizi na hujuma hizo tunaweza kuashiria ugaidi wa kiserikali na vitisho dhidi ya umoja wa kieneo.

Rais Miguel Diaz-Canel wa Cuba

Kwa upande wake Rais Nicolas Maduro wa Venezuela mbali na kulaani vikwazo vya Marekani dhidi ya Caracas amesema kuwa, nchi yake ina katika sekta ya viwanda na kipato cha kuweza kukabiliana na vikwazo na hivyo kufikia uthabiti na ustawi wa kweli wa kiuchumi na hatimaye kulinda haki za kijamii za wananchi wa nchi hiyo.

Kile ambacho kiko wazi katika wakati huu ni kwamba, kuheshimu sheria, haki ya kuchagua, mamlaka ya kujitawala na uhuru wa mataifa ni mambo ambayo yanapingana kabisa na siasa za kimabavu na za kupenda kujitanua za Washington. Kwa msingi huo basi inaonekana kuwa, viongozi wa Marekani licha ya kufanyya juhudi nyingi, lakini wanapaswa kukiri juu ya kugonga mwamba juhudi zao za kutaka kutoa pigo kwa Venezuela na Cuba, kwani kusimama kidete mtawalia mataifa hayo kunaonyesha dhahiri shahiri kwamba, siasa za kibabe na za kupenda kujitanua za Marekani zimeshindwa na kugonga ukuta.

Tags