Wamarekani waandamana kulaani uchu wa vita wa utawala wa Trump
Maelfu ya wanaharakati na wananchi wa Marekani wamefanya maandamano katika makumi ya miji ukiwemo mji mkuu Washington, kulaani hatua ya utawala wa Donald Trump ya kumuua shahidi kamanda wa jeshi la Iran, Luteni Jenerali Soleimani, pamoja na hatua ya Washington ya kutuma maelfu ya askari katika eneo la Asia Magharibi.
Mamia ya waandamanaji walikusanyika jana Jumamosi nje ya hoteli mashuhuri ya Trump mjini Washington wakiwa na mabango yaliyoandikwa, "Hatutaki vita na vikwazo dhidi ya Iran."
Maandamano zaidi ya 70 yaliyoshuhudiwa jana katika miji mbalimbali ya Marekani, yalipangwa na makundi ya wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu ambao wanapinga vikali hatua yoyote ya Washington ya kuanzisha vita na Iran.
Mbali na Washington, maandamano hayo yameshuhudiwa katika miji mikubwa ya Marekani ikiwemo ya Miami, Tampa, Philadelphia, San Francisco na New York.
Mamia ya waandamanaji katika Medani ya Times wamesikika wakipiga kelele wakisema "Tunataka amani sasa" na wengine wakisema "Marekani ondoka Mashariki ya Kati."
Katika jiji la Minneapolis, waandamanaji walikusanyika karibu na Chuo Kikuu cha Minnesota wakipinga hatua hizo za kichokozi na kichochozi za Washington. Meredith Aby, Mwenyekiti wa Kamati ya Kupinga Vita aliyeshiriki maandamano hayo mjini Minneapolis amesema, "Tunapaswa kuanza kuondoka Iraq, sio kutuma maelfu ya askari zaidi. Tunapaswa kuzima uhasama kati yetu na Iran, sio kumwaga petroli kwenye moto."