UK: Umoja wa Ulaya utaendelea kuheshimu mapatano ya nyuklia ya JCPOA
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza alisema jana Ijumaa baada ya kikao cha dharura cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels Ubelgiji kwamba, nchi yake pamoja na Umoja wa Ulaya wataendelea kuheshimu mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
Andrew Murrison ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya bado wanaendelea na msimamo wao wa kupunguzwa haraka mivutano katika eneo la Asia Magharibi.
Kikao cha dharura cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya kilifanyika jana Ijumaa katika mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels, kwa kuhudhuriwa na wajumbe kutoka nchi wanachama.
Masuala yaliyopelekea kuitishwa kikao hicho cha dharura ni pamoja na uamuzi wa Iran wa kuanza kutekeleza awamu wa tano ya kupunguza ahadi zake ndani ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, kuongezeka wasiwasi kati ya Iran na Marekani baada ya serikali ya Donald Trump kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Quds, cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, na ajali ya ndege ya Ukraine iliyotokea karibu na Tehran.
Itakumbukwa kuwa, baada ya rais wa Marekani kujitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, nchi hiyo imetengwa kikamilifu kiasi kwamba hata waitifaki wa karibu kabisa wa Marekani kama vile Uingereza, Ujerumani na Ufaransa, zote zimekataa katakata mwito wa rais wa Marekani wa kujitoa kwenye makubaliano hayo ya kimataifa.