Nchi za Ulaya haziwasaidii wakimbizi wanaozama baharani
Nchi za Ulaya hazijachukua hatua za kutosha kuwanusuru wakimbizi wanaozama baharini wakijaribu kufika barani Ulaya kwa njia hatari za baharini.
Shirika la kutoa misaada la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limesema limelazimika kuanza kutoa huduma za kuwanusuru wakimbizi katika Bahari ya Mediterranea baada ya nchi za Umoja wa Ulaya kusitisha oparesheni za uokozi mwezi Januari.
MSF imesema wakimbizi wako katika hatari ya kughiriki kutokana na kutumia njia hatari za baharini kati ya Afrika Kaskazini na Ulaya hasa katika msimu huu wa machipuo na msimu ujao wa joto kali.
Mkuu wa masuala ya kimataifa katika MSF Joanne Liu amesema kukosekana suluhisho la kimataifa kuhusu mgogoro wa wakimbizi pamoja na nchi za Ulaya kukataa kutoa njia mbadala za kutumiwa na wakimbizi kuvuka bahari ni jambo ambalo limepelekea maelfu ya wakimbizi waendelee kupoteza maisha.
Wakimbizi na wahajiri karibu 1,000 wamepoteza maisha mwaka huu wa 2016 wakijaribu kuingia Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranea.
Mwaka 2015 karibu wakimbizi milioni moja waliingia Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranea huku wengine 3,700 wakipoteza maisha au kutoweka katika safari hiyo hatari. Aghalabu ya wakimbizi hao wanakimbia vita nchini Iraq na Syria huku wengine wakiwa ni wakimbizi wa kiuchumi kutoka nchi za Afrika.