Aug 22, 2024 02:18 UTC
  • Umoja wa Mataifa wapongeza ukarimu wa Iran kwa wakimbizi

Afisa msimamizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR hapa nchini Iran ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu kwa kuwapokea kwa ukarimu na kuwa mwenyeji wa wakimbizi.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya na Elimu ya Tiba ya Iran, Inna Gladkova mwakilishi wa UNHCR hapa nchini amesema taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa inaishukuru Jamhuri ya Kiislamu kwa huduma za matibabu inazozitoa kwa wakimbizi.

Amesema Iran ni moja ya nchi kubwa duniani katika kuwahifadhi wakimbizi. Katika miongo minne iliyopita, UNHCR imeshirikiana na Jamhuri ya Kiislamu katika miradi ya pamoja kuhusiana na masuala ya wakimbizi.

Gladkova ameashiria elimu ya wakimbizi nchini Iran na kueleza kuwa, watoto wote wa Afghanistan wanafurahia fursa sawa ya kupata elimu kama wanafunzi wa Iran.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza msimamo wa serikali ya Tehran wa kuendelea kuwahifadhi kwa ukarimu wahajiri na wakimbizi huku ikikanusha madai yanayotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusiana na kushinikizwa wakimbizi na raia wa kigeni nchini.

Makadirio yaliyofanywa kuhusu idadi ya wakimbizi wa Kiafghani waliopo nchini Iran ni zaidi ya milioni 5. Wakimbizi wa Kiafghani ambao wana uhusiano wa kiutamaduni, kihistoria na kidini na wananchi wa Iran hadi sasa wameweza kustafidi na suhula na huduma zote zinazotolewa na serikali ya Iran sawa kabisa na wananchi wa Iran.  

Tags