Seneti ya Pakistan yapasisha azimio dhidi ya Muamala wa Karne
(last modified Wed, 19 Feb 2020 08:18:26 GMT )
Feb 19, 2020 08:18 UTC
  • Seneti ya Pakistan yapasisha azimio dhidi ya Muamala wa Karne

Baraza la Seneti la Pakistan limepasisha kwa kauli moja azimio la kulaani mpango wa Kimarekani wa Muamala wa Karne, likisisitiza kuwa njama hizo za Washigton zilizojaa hila zinakusudia kuwafanya Wapalestina wasalimu amri katika hali ya idhilali mbele madhalimu wao.

Rasimu ya azimio hilo iliyowasilishwa na Seneta Mushtaq Ahmad Khan wa chama cha Jamaat-e-Islami imepasishwa kwa kishindo na bunge hilo la juu la Pakistan lenye viti 104.

Azimio hilo limesema kuna haja ya kutafuta suluhu yenye haki, usawa na uadilifu kwa kadhia ya Palestina, na itakayooana na maazimio ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la umoja huo.

Kadhalika azimio hilo lililopasishwa na Seneti ya Pakistan limeitaka serikali ya Islamabad kuitisha kikao cha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC, kitakachojadili stratajia inayokubalika na pande zote, na itakayolinda haki na maslahi halali ya taifa la Palestina.

Maandamano ya Wapakistan huku wakichoma kwa moto bendera za Israel na US

Itakumbukwa kuwa tarehe 28 mwezi uliopita wa Januari Rais Donald Trump wa Marekani na Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu walizindua mpango huo eti wa amani wa Muamala wa Karne katika ikulu ya White House.

Waislamu na wapenda haki katika kila pembe ya dunia wanaendelea kulaani na kuukosoa mpango huo wa kidhalimu wa Kimarekani na Kizayuni unaokanyaga haki za taifa la Palestina.

Tags