Guterres asema yuko tayari kutuma ujumbe kaskazini mwa Syria
(last modified Sun, 01 Mar 2020 02:40:52 GMT )
Mar 01, 2020 02:40 UTC
  • Guterres asema yuko tayari kutuma ujumbe kaskazini mwa Syria

Kufuatia kushtadi mizozo katika eneo la kaskazini mwa Syria, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres ametangaza utayarifu wake kwa ajili ya kutuma ujumbe wa umoja huo katika mkoa wa Idlib, kaskazini mwa nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na katibu mkuu huyo wa UN imesema kuwa, lengo la kutumwa ujumbe huo kaskazini mwa Syria ni kuchunguza hali ya mkoa wa Idlib. Ameongeza kwamba hitajio kubwa kwa Syria ni kufikiwa usitishaji vita wa haraka kabla ya hali ya mambo haijatoka kwenye udhibiti. Katika wiki za hivi karibuni, mkoa wa Idlib, umeshuhudia mapigano makali kati ya jeshi la serikali na magaidi wanaoungwa mkono na baadhi ya nchi za kigeni hususan Uturuki.

Uturuki, muungaji mkono mkubwa wa makundi ya kigaidi yanayotenda jinai

Kuendelea kusonga mbele jeshi la Syria kwa lengo la kuyakomboa maeneo ambayo ni ngome za mwisho za makundi ya kigaidi katika mikoa ya Idlib na Aleppo, kaskazini magharibi mwa Syria, kumeibua mzozo kati ya serikali ya Ankara na Damascus. Uturuki sambamba na kupinga operesheni hizo za jeshi la Syria, imeyakalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya nchi hiyo, huku ikiendelea kutoa uungaji mkono kwa magaidi. Katika uwanja huo serikali ya Damascus imesisitiza kwamba haitoiruhusu Uturuki iendelee kuyaunga mkono makundi ya kigaidi dhidi yake. Russia iko nchini Syria kupitia mwaliko rasmi wa serikali ya Damascus kwa ajili ya kutekeleza operesheni za kijeshi za kuyatokomeza makundi hayo ya kigaidi.