Radiamali ya Venezuela baada ya Marekani 'kumshtaki' Rais Maduro
(last modified Fri, 27 Mar 2020 08:01:28 GMT )
Mar 27, 2020 08:01 UTC
  • Radiamali ya Venezuela baada ya Marekani 'kumshtaki' Rais Maduro

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amekosoa vikali na kutaja kama kichekesho hatua ya Marekani ya eti kumfungulia mashitaka ya ulanguzi wa mihadarati, ambapo amemtaja rais wa nchi hiyo, Donald Trump kuwa mtu mbaguzi.

Maduro amesema yuko tayari kutumia njia zote zinazohitajika kukabiliana na uvamizi tarajiwa wa Marekani na Colombia katika nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Huku akimhutubu rais huyo wa Marekani katika hotuba yake kwa njia ya televisheni, Rais Maduro amesema, "Donald Trump, wewe ni mtu uliyepigika na matatizo, huzuni na msongo wa mawazo. Unaendesha uhusiano wa kimataifa kama mafia na msanii wa utapeli wa New York namna ulivyokuwa enzi zako za biashara ya kuuza majumba."

Rais wa Venezuela amejibu vitisho vya Marekani vya kuivamia kijeshi nchi hiyo ya Amerika ya Latini kwa kushirikiana na nchi muitifaki na kusema, "iwapo siku moja utawala wa kiimla (Marekani) na vikaragosi vyao (Colombia) watathubutu kugusa japo unywele wetu mmoja, watakabiliana na ghadhabu zetu Wabavaria, na taifa hili zima litawafuta (wavamizi) wote katika uso wa dunia."

Marais Trump na Maduro

Kabla ya hapo, Jorge Arreaza, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela alisema kitendo hicho cha watawala wa Washington cha eti kumfungulia Rais Maduro mashitaka ya ulanguzi wa dawa za kulevya kinaonyesha ni jinsi gani watawala wa Washington wamekata tamaa, na kusisitiza kuwa, "Trump kwa mara nyingine tena amelihujumu taifa la Venezuela na taasisi zake za kidemokrasia, kwa kutumia mfumo mpya wa mapinduzi na kwa kutumia madai yasiyo na msingi, ya kipuuzi na chafu." 

Hapo jana Marekani ilitangaza zawadi ya dola milioni 15 kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazopelekea kukamatwa na kushitakiwa Maduro, ambaye Washington inamtuhumu pamoja na mawaziri wa ngazi za juu wa nchi hiyo kuwa wanaongoza kundi la walanguzi wa mihadarati aina ya cocaine.

Tags