Maseneta wa Marekani watishia 'kuichukulia hatua' Saudia
Maseneta wa Marekani wametishia kuangalia upya uhusiano wao na Saudi Arabia kutokana na hatua ya Riyadh ya kuendelea kuvutana na Russia juu ya bei ya mafuta ghafi ambayo imeiathiri pia Marekani.
Maseneta hao 13 wanaotoka katika majimbo yanayozalisha mafuta nchini Marekani wametishia kuwa, ikilazimu watauchukulia hatua utawala wa Riyadh.
Mwezi uliopita, maseneta hao walizungumza kwa njia ya simu na balozi wa Saudia nchini Marekani, Bintimfalme Reema Bint Bandar Aal Saud na kumwambia, "hatutatizama upya tu uhusiano wetu na Riyadh, lakini pia tutachukua hatua."
Huku akisimuliwa yaliyojiri katika mazungumzo hayo ya simu, Seneta Dan Sullivan wa Alaska ameiambia televisheni ya CNN kuwa, iwapo (maseneta hao) wataangalia upya uhusiano na Riyadh ambao wengi wao wamekuwa wakiuunga mkono, basi kitendo hicho kitakuwa na athari mbaya katika uhusiano wa muda mrefu wa Riyadh na Washington.
Bei ya mafuta katika soka la dunia imeporomoka kwa asilimia 59 kutokana na vita vya bei ya bidhaa hiyo baina ya Russia na Saudi Arabia.
Kiwango hiki cha sasa cha kushuka bei ya mafuta duniani hakijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 18 iliyopita.
Maseneta hao wa majimbo yanayozalisha mafuta ya Marekani wanatazamiwa Jumamosi kumpigia simu Khalid al-Falih, Waziri wa Nishati wa Saudia ili kushinikiza kupatikana ufumbuzi wa mgogoro wa kushuka kwa bei ya bidhaa hiyo duniani.