WFP: Njaa kuikumba zaidi dunia kutokana na maradhi ya Covid-19
Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) limetangaza katika taarifa yake kwamba idadi ya watu wanaokabiliwa na ukosefu wa chakula inaweza kuongezeka maradufu mwaka huu wa 2020 na kufikia watu milioni 265 kutokana na maradhi ya Covid-19.
Shirika la WFP limeeleza kuwa, athari ilizosababishwa na kukosa mapato katika sekta ya utalii, kusitishwa safari na vizuizi vingine kutokana na maambukizi ya virusi vya corona inaweza kuwapelekea watu wasiopungua milioni 130 kukumbwa na njaa mwaka huu.
Mchumi Mkuu na Mkurugenzi wa Utafiti, Tathmini na Udhibiti wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani Arif Husain amesema kuwa maradhi ya Covid-19 ni hatari kwa mamilioni ya watu duniani katika kipindi hiki ambacho maambukizi ya virusi vya corona yanaenea kwa kasi. Ameongeza kuwa nchi zote zinapaswa kushirikiana kwa ajili ya kushughulikia suala hili. Amesema gharama zitakuwa za juu sana na watu wengi watapoteza maisha iwapo hatua za pamoja hazitachukuliwa katika uwanja huo.

Shirika la WFP linataraji kuomba msaada wa dola kuanzia bilioni 10 hadi 12 katika mwaka huu wa 2020 ili kukidhi mahitaji ya chakula katika nchi mbalimbali duniani.
Hata kabla ya maambukizi ya corona kuiathiri dunia, nzige wa jangwani pia walikuwa tayari wameharibu mazao huko mashariki mwa Afrika na kusababisha ongezeko la watu wanaohitaji msaada wa chakula katika nchi kadhaa za eneo hilo.