WHO: Kulegezwa vizuizi vya watu kubaki majumbani kutaibua changamoto
Wakati idadi ya watu waliougua ugonjwa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya corona ikifikia zaidi ya milioni 4 duniani kote, Shirika la Afya Duniani, WHO limesema, hatua ya baadhi ya nchi kulegeza vizuizi vya watu kubakia majumbani imeonesha baadhi ya changamoto zitakazoyakabili mataifa siku za usoni.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi katika moja ya mikutano yake ya kutoa muhtasari wa hali ya COVID-19 duniani, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom amesema, mwishoni mwa wiki zimeshuhudiwa dalili za changamoto zinazoweza kuikabili dunia baada ya hatua zilizochukuliwa na Korea Kusini, China na Ujerumani za kulegeza masharti ya kubakia majumbani, ambako maambukizi mapya yamejitokeza.
Dokta Adhanom amezungumzia pia uamuzi wa baadhi ya nchi kutaka kufungua shule ili watoto warejee kwenye mafunzo ambapo amesema: "Kuhusu watoto kwenda shule, wanaochukua uamuzi lazima waangalie idadi ya mambo kadhaa kama watafikia uamuzi wa kufungua au kutofungua shule. Kwanza, ni uelewa wa dhati kuhusu maambukizi ya sasa ya COVID-19 na kiwango cha athari za virusi hivyo kwa watoto, pili mwenendo wa COVID-19 kule ambako shule inapatikana lazima ufahamike. Na tatu, uwezo wa kudhibiti COVID-19 na mikakati ya kukinga watoto shuleni.”

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, amepongeza pia nchi ambazo zimetumia kipindi cha watu kubakia majumbani kama njia ya kuimarisha mbinu za upimaji, ufuatiliaji, kuwatenga na kuhudumia wagonjwa, njia ambazo amesema ni muhimu katika kukabili kasi ya virusi vya Corona na hivyo kupunguza mzigo kwa mfumo wa afya.
Amesema ni wazi kuwa vizuizi vimekuwa na athari katika njia za watu kujipatia kipato, hivyo ulegezaji wowote wa vizuizi hivyo ni lazima uende sambamba na kuwa macho ili kuhakikisha mbinu za kulinda kipato zinakwenda sambamba na mbinu za kutunza afya.../