Marekani ya Trump; nembo na mshirika wa ugaidi wa kiserikali ulimwenguni
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Marekani ni nembo ya ugaidi wa kiserikali na kueleza kwamba, historia ya nchi hiyo katika kuunga mkono ugaidi iko wazi kabisa.
Sayyid Abbas Mousavi amesema hayo katika radiamali yake dhidi ya madai ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani katika uga wa kupambana na ugaidi na kusema bayana kwamba, kutokana na Washington kuwa na historia kongwe ya kuyadhamini na kuyapatia fedha na silaha makundi mbalimbali ya kigaidi, kutekeleza kwake ugaidi wa kiserikali na kuuunga mkono waziwazi utawala wa Israel unaofanya mauaji kila leo dhidi ya Wapalestina, nchi hiyo katu haiwezi kuwa kipimo kizuri cha kutathmini juhudi zilizofanyika kwa ajili ya kupambana na ugaidi.
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani imedai kwamba, eti Iran imekuwa haitoi ushirikiano kwa Washington katika kupambana na ugaidi na kwamba, eti serikali ya Tehran imeendelea kuunga mkono ugaidi.
Tukitupia jicho kwa haraka haraka sera na siasa za Marekani katika eneo la Asia Magharibi tunashuhudia wazi, himaya na uungaji mkono wa Washington kwa utawala haramu wa Israel na kisha hatua yake ya kutekeleza ugaidi wa kiserikali mpaka ugaidi wa kiafya dhidi ya Iran. Ukweli ulio wazi ni kuwa, Marekani imekuwa ikiunga mkono moja kwa moja ugaidi na wakati huo huo imekuwa na muamala wa kigaidi na mataifa ambayo yanapigania kujitawala na yasiyokubali kuburuzwa au kuamrishwa na dola hilo la kibeberu.
Hapana shaka kuwa, baada ya utawala haramu wa Israe, Marekani ni utawala wa pili ulimwenguni ambao umekuwa ukitangaza rasmi kwamba, unatumia suhula za serikali na vikosi vyake vya ulinzi kwa ajili ya kutekeleza operesheni za kigaidi na itaendelea na mbinu na njia hiyo.
Himaya na uungaji mkono wa Marekani kwa utawala katili wa Israel, ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 70 sasa, utawala ambao umeweka katika ajenda zake suala kuwaua wananchi madhlumu wa Palestina, shakhsia wa kisiasa na makamanda wa muqawama ni hatua zinazounga mkono na kuthibitisha ugaidi wa kiserikali wa Washington.
Hatua ya Marekani ya kutoa amri ya kuuawa Luteni Jenerali Qassim Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa vikosi vya muqawama katika eeo la Asia Magharibi, nayo ni nembo na kielelezo cha wazi cha Washington kuendesha ugaidi wa kiserikali ambao hauna mipaka. Kuuawa na Marekani katika ardhi ya Iraq Luteni Jenerali Qassim Soleimani aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH), kulifunua pazia la ugaidi ulioratibiwa na wa kiserikali wa Marekani ambao kimsingi unakiuka wazi na bayana sheria za kimataifa.
Katika uwanja huo, Gholamhossein Ismaili, msemaji wa Vyombo vya Mahakama vya Iran anasema: Hatua ya serikali inayotenda jinai ya Marekani ya kumuua shahidi Luteni Jenerali Qassim Soleimani na Abu Mahdi al-Mohandis, aliyekuwa Naibu Mkuu wa Jeshi la Kujitolea la Wananchi wa Iraq la Al-hashdu-Sha'abi kwa upande wa kisheria, ni hatua ya kigaidi na mfano wa wazi kabisa wa ugaidi wa kiserikali.
Mbali na ugaidi wa kiserikali, hatua za Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Iran kuanzia vikwazo vya kiuchumi hadi vikwazo vya dawa na suhula pamoja na zana za tiba ni mfano na misdaqi ya wazi ya muamala wa kigaidi. Vikwazo vya dawa na suhula nyingine za kitiba, ni tishio la moja kwa moja dhidi ya uhai wa wanadamu na jambo hilo linakiuka dhahir shahir msingi mkuu na muhimu kabisa wa haki ya mwanadamu ambao unahesabiwa kuwa ni jiwe la msingi la haki nyingine za binadamu.
Katika mazingira kama haya, hatua za kisiasa, kijeshi na kiuchumi za serikali ya Marekani dhidi ya taifa la Iran ambazo zina ishara za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja za ugaidi bila shaka zinaikosesha nafasi White House ya kuwa kipimo kizuri cha kutathmini juhudi za mataifa mengine zilizofanyika kwa ajili ya kupambana na ugaidi.
Msururu wa mafaili ya Marekani katika kuutazama ugaidi kwa jicho la wenzo wa kufikia malengo yake katika eneo la Asia Magharibi hususan huko Syria na Iraq, kunaiondoa kabisa nchi hiyo katika orodha ya nchi zinazopambana na ugaidi; kwani badala ya kuwajibika mkabala na kuongezeka makundi ya kigaidi, imemuua kigaidi kamanda halisi wa vita dhidi ya ugaidi yaani Shahidi Luteni Jenerali Qassim Soleimani.