May 27, 2020 03:50 UTC
  • Picha za satalaiti zaonyesha nyumba za Waislamu wa Mynamar zikichomwa moto

Shirika la kutetea haki za binadmau la Human Rights Watch (HRW) limetoa mwito wa kufanyika uchunguzi baada ya picha za satalaiti kuonyesha nyumba za Waislamu katika mkoa wa Rakhine nchini Mynamar zikiteketea kwa moto.

Katika taarifa ya jana Jumanne, shirika hilo limesema kuna haja ya kuanzishwa uchunguzi haraka iwezekanavyo ili kuwabaini na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria waliohusika na jinai hiyo ya kuchoma moto nyumba zaidi ya 200 katika kijiji cha Let Kar, mjini Mrauk-U uliopo katika jimbo la Rakhine, magharibi mwa Myanmar.

Hii ni katika hali ambayo, duru za habari nchini humo zimeripoti kuwa, kijiji hicho cha Waislamu wa jamii ya Rohingya kiliteketezwa moto kwa makusudi na askari wa serikali mnamo Mei 16 mwaka huu.

Hakuna maelezo yoyote yaliyotolewa hadi sasa kuhusu watu waliopoteza maisha au kujeruhiwa kwenye jinai hiyo ambayo ni katika mfululizo wa dhulma zinazofanywa na jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu Warohingya tokea mwaka 2017.

Vijiji vya Waislamu wa Rohingya vimekuwa vikichimwa moto tokea 2017

Hivi karibuni Human Rights Watch ilisema jinai zinazotekelezwa na Myanmar hazipaswi kulaaniwa tu kwa maneno bali dunia inapaswa kuchukua hatua za kivitendo kukabiliana na hali hiyo.

Itakumbukwa kuwa wimbi jipya la mauaji, mashambulizi na ubakaji wa jeshi la Myanmar katika mkoa wa Rakhine kuwalenga Waislamu wa Rohingya, lilianza tarehe 25 Agosti mwaka 2017 ambapo zaidi ya Waislamu elfu sita waliuawa na wengine elfu nane kujeruhiwa, mbali wengine milioni moja kulilazimika kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh wakitoroka ukatili huo wa jeshi la Mynamar likishirikiana na Mabudha wenye misimamo ya kufurutu ada.

Tags