Baada ya vitisho, hatimaye Trump akata uhusiano na WHO
https://parstoday.ir/sw/news/world-i61298-baada_ya_vitisho_hatimaye_trump_akata_uhusiano_na_who
Rais Donald Trump wa Marekani ametangaza kukata uhusiano na Shirika la Afya Duniani WHO, akidai kuwa taasisi hiyo ya kimataifa ni kikaragosi cha China.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 30, 2020 03:40 UTC
  • Baada ya vitisho, hatimaye Trump akata uhusiano na WHO

Rais Donald Trump wa Marekani ametangaza kukata uhusiano na Shirika la Afya Duniani WHO, akidai kuwa taasisi hiyo ya kimataifa ni kikaragosi cha China.

Katika kikao na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House jana Ijumaa, Trump alikariri tuhuma zake za kichochezi dhidi ya shirika hilo akidai kwamba linaipendelea China, na eti lilishindwa kushughulikia ipasavyo janga la corona.

Aidha alitumia jukwaa hilo kuipaka China matope tena kwa kusema: Dunia inahitaji majibu kutoka kwa China juu ya virusi (vya corona). Lazima wawe wazi.

Trump amechukua uamuzi huo chini ya wiki mbili baada ya kumuandikia barua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Dunia, Tedros Adhanom Gabrayesus ambapo alidai kuwa, "Marekani itaikatia misaada WHO kikamilifu iwapo haitapiga hatua kubwa za kujiboresha ndani ya siku 30 zijazo."

Trump amekuwa akitoa kauli za kugongana na kulaumiana kwa janga la corona

Katika barua hiyo ya vitisho kwa Mkurugenzi Mkuu wa WHO na ambayo ilikosolewa vikali katika kona mbalimbali za dunia, Trump alisema "tunaipa WHO dola milioni 450 kila mwaka, lakini hawatutendei wema, wamekuwa wakitupa ushauri mbaya."

Wadadisi wa mambo wanaamini kuwa, lengo la Rais huyo wa Marekani kuzilaumu WHO na China kwa janga la corona, ni kuficha uzembe wa serikali yake ulioifanya Marekani iwe muathirika mkubwa zaidi wa mlipuko wa corona duniani.