Macron apinga kushambuliwa nembo za kikoloni
Kufuatia kuenea maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi na utaifa huko Marekani ambapo wimbi lake limeenea pia barani Ulaya; wafanya maandamano na wale wote wanaopinga vitendo hivyo vya ubaguzi wameshambulia nembo mbalimbali za kikoloni katika nchi mbalimbali duniani ambazo kwa karne kadhaa zilipelekea raia weusi kutumiwa kama watumwa katika nchi za Magharibi. suala hilo limepingwa na baadhi ya wakuu wa Ulaya akiwemo Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa.
Huko Ufaransa aghlabu ya waandamanaji wametaka kuondolewa sanamu za sura za watu mbalimbali ambao walikuwa chanzo katika kutekelezwa vitendo vya ubaguzi wa rangi, biashara ya utumwa au walikuwa na nafasi katika zama za ukoloni huko Ufaransa. Wafanya maandamano katika mji wa Lille, Paris na katika ardhi za ....wametaka kung'olewa masanamu ya baadhi ya wanasiasa wa zama wa ukoloni kama sanamu la Kulber lililoko mkabala na bunge la taifa la Ufaransa. Hii ni kwa sababu mwanasiasa huyo anatambuliwa kama nembo ya uporaji, jinai na mienendo isiyo ya kibinadamu wakati wa ukoloni nchini Ufaransa. Maandamano yalianza katika mji wa Lille wakilalamikia sanamu la Jenerali Louis Léon César Faidherbe ambaye alikuwa na mchango mkubwa katika ukoloni nchini Senegali. Katika maeneo ya kama ya kisiwa cha Reunion wafanya maandamano wametaka kuteremshwa chini sanamu la Labordonne mtawala wa zamani wa kisiwa hicho ambaye alikuwa na nafasi kuu katika biashara ya utumwa.
Akijibu hatua hiyo, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amedai kuwa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi hayapasi kuandika tena historia ya chuki. Macron ametamka hayo ikiwa ni radiamali yake kwa mashambulizi yanayoendelea kufanywa na waandamanaji katika nchi mbalimbali kufuatia kuuliwa kikatili huko Marekani, George Floyd, Mmarekani mwenye asili ya Afrika na kushambuliwa masanamu ya watu wenye mfungamano na utumwa au wavunjaji wengine wa haki za binadamu. Akihutubia kwa njia ya runinga Macron ameeleza kuwa nchi ya Ufaransa haitafuta katika historia yake jina lolote lile. Ufaransa haitasahau kazi yake yoyote ya sanaa na haitatremsha chini sanamu lolote."

Amesisitiza kuwa Jamhuri ya Ufaransa haitafungua misumari katika nembo za masanamu ya biashara ya utumwa na yale yanayodhihirisha kuwa wazungu ni bora kuliko raia weusi. Msimamo huo wa kibaguzi wa Macron mkabala na wiki tatu za maandamano dhidi ya ubaguzi wa rangi na ukatili huko Marekani na wiki mbili za maandamano mengine kama hayo nchini Ufaransa yamekabiliwa na ghadhabu na hasira kubwa za wananchi. Baadhi ya wanasiasa, wasanii na wanaharakati wanaopiga vita ubaguzi wa rangi pia wamelaani matamshi hayo ya kifedhuli na ya kikoloni ya rais huyo wa Ufaransa.
Hii ni katika hali ambayo huko nyuma Rais Macron wa Ufaransa yaani mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka jana akiwa ziarani nchini Kodivaa (Ivory Coast) koloni la zamani la Ufaransa barani Afrika alisisitiza kuwa kadhia ya ukoloni ilikuwa ni kosa baya na kutaka kubadilishwa kurasa hizo za historia. Rais Macron aidha alisema akiwa huko Abdijan mji mkuu wa Kodivaa kwamba: Aghalabu ya watu wanaichukulia Ufaransa kuwa nchi iliyokuwa na mitazamo ya kibeberu na kuiona kuwa iliyotumbukia katika ukoloni; jambo alilolilotaja kuwa ni kosa kubwa na lenye kukiuka maadili ya Jamhuri ya Ufaransa. Wakati wa kampeni zake za uchaguzi pia, Rais huyo wa Ufaransa alikabiliwa na wimbi la ukosoaji pale aliposema kuwa ukoloni wa Ufaransa nchini Algeria ilikuwa ni jinai dhidi ya binadamu. Hata hivyo hivi sasa anasisitizia ulazima wa kulindwa nembo za kibaguzi na kikoloni na utambulisho wake ikiwemo biashara ya utumwa. Ni wazi kuwa kwa matamshi yake hayo, Macron ameunga mkono waziwazi ukoloni wa nchi za Ulaya kama Ufaransa, Uingereza na Ubelgiji barani Afrika kinyume na misimamo yake ya huko nyuma.
Boris Johnson Waziri Mkuu wa Uingereza pia amechukua msimamo sawa na huo katika kukabiliana na mashambulizi ya waandamanaji dhidi ya ubaguzi wa rangi wanaoshambulia nembo za kikoloni nchini humo. Johnson ameeleza kuwa: Maandamano ya kuonyesha mshikamano na George Floyd raia Mmarekani mwenye asili ya Afrika yamekengeuka mkondo wake; na wahusika wake wanapasa kuchukuliwa hatua. Katika hali ambayo maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi na ukatili katika siku za hivi karibuni yameshuhudiwa huko Uingreza huku waandamanaji wakiitaja nchi hiyo kama ya kibaguzi; Msemaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza ametangaza kuwa Boris Johnson hatambui Uingereza kama nchi baguzi na kukitaja kitendo cha kung'olewa sanamu la Edward Colston mmoja wa vigogo wa biashara ya utumwa wa nchi hiyo katika karne ya 17 kuwa ni uhalifu usiokubalika. Huko nyuma pia katika makala moja iliyochapishwa mwaka 2002 Boris Johnson aliunga mkono kikamilifu ukoloni wa Uingereza hususan barani Afrika. Johson aliandika katika makala hiyo kuwa: Suala la ukoloni lisingepasa kabisa kumalizika huko Afrika na wakati huo huo akapuuza nafasi ya nchi hiyo katika biashara hiyo ya utumwa.
