Bachelet: Ubaguzi wa rangi nchini Marekani unasikitisha
-
Michelle Bachelet
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema anasikitishwa sana na ubaguzi wa rangi wa kimfumo nchini Marekani.
Michelle Bachelet ambaye alikuwa akihutubia mkutano wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ameeleza kusikitishwa sana na ubaguzi wa rangi wa kimfumo nchini Marekani na vilevile ukatili wa polisi dhidi ya watu wanaofanya maandamano ya amani na amesisitiza udharura wa kuchukuliwa hatua za kivitendo za kurekebisha idara ya polisi na mahakama za Marekani katika masuala yanayohusiana na ubaguzi na ukatili dhidi ya jamii za waliowachache.
Kwa upande wake mwakilishi wa Marekani katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Andrew Bremberg amekiri katika mkutano huo kwamba kuna mapungufu na nakisi nyingi katika masuala ya haki za binadamu nchini kwake na amedai kuwa, Washington inaahidi kuondoa nakisi na mapungufu hayo yanayohusiana na ubaguzi wa rangi.

Nchi 54 za Kiafrika zilikuwa zimelitaka Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kushughulikia suala la ubaguzi wa rangi unaofanywa na polisi ya Marekani na mienendo ya kikatili dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika.
Inatazamiwa kuwa, Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa litatayarisha muswada wa kuundwa kamisheni ya uchunguzi kuhusu ubaguzi wa rangi wa kimfumo na sulubu zinazowapata Wamarekani wenye asili ya Afrika.
Hatua hii imechukuliwa baada ya polisi mzungu kumuua kikatili Mmarekani mweusi, George Floyd katika mji wa Mineapolis tarehe 24 mwezi uliopita.