Mapigano na ghasia zasababisha watu milioni 80 kuwa wakimbizi
Umoja wa Mataifa umesema takriban watu milioni 80 (asilimia 1 ya jamii ya mwanadamu) wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi zao kutokana na vita na mapigano katika kona mbalimbali za dunia.
Ripoti mpya ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR iliyotolewa jana Alkhamisi kwa mnasaba wa Siku ya Wakimbizi Duniani itakayoadhimishwa kesho Jumamosi (Juni 20) imeashiria ongezeko la wakimbizi milioni 9 waliofurushwa makwao kutokana na mapigano katika sehemu mbalimbali duniani mwaka jana 2019, ikilinganishwa na mwaka juzi 2018.
Ripoti hiyo ya UNHCR imesema ongezeko hilo la wakimbizi hadi milioni 80 ni maradufu ya idadi ya wakimbizi wote duniani ya milioni 41 mwaka 2010.
Kamishna Mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi ameeleza kushtushwa na kusikitishwa kwake na ongezeko hilo la wakimbizi katika pembe mbalimbali za dunia kutokana na vita, mapigano na ghasia.
Amesema asilimia 68 ya wakimbizi wote duniani wanatoka katika nchi tano tu ambazo ni Syria, Venezuela, Afghanistan, Sudan Kusini na Myanmar.
Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa amesema nchi za dunia zinapaswa kuendelea kuwapa hifadhi wakimbizi wanaoihitaji, licha ya janga la corona ambalo limepelekea aghalabu ya nchi duniani kufunga mipaka yao.