UN: Umoja wa Ulaya hauwezi kusimamia mgogoro wa wakimbizi
Kamishna Mkuu wa Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa amekosoa utendaji wa Umoja wa Ulaya na udhaifu wa nchi wanachama katika umoja huo katika suala la kufikia mapatano ya kutatua mgogoro wa wakimbizi.
Filippo Grandi ameliambia jarida la kila wiki la Spiegel la Ujerumani kwamba: "Moja ya maeneo tajiri zaidi duniani haliwezi kujisimamia na kushughulikia masuala yake lenyewe, na mimi ninapoteza subira yangu kuhusu na Ulaya hatua kwa hatua."
Kamishna Mkuu wa Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa amesema hali ya mambo katika eneo la Idlib huko Syria inatokota na kusisitiza kuwa, Umoja wa Mataifa unahitaji bajeti ya Euro bilioni 10 na kwamba fedha hizo zitatumika kuwasaidia watu wa Syria hususan wakimbizi. Amesema eneo la Idlib peke yake lina wakimbizi milioni 2.5 na kimsingi karibu wakazi wote wa eneo hilo wanahitajia misaada.
Afrisa huyo wa Umoja wa Mataifa ameashiria maambukizi ya virusi vya corona na athari zake mbaya na kusema: Ulaya inapaswa kujitayarisha kwa ajili ya hujuma ya idadi kubwa ya wakimbizi. wa
Filippo Grandi amesema kuwa, miongoni mwa athari mbaya za maambukizi ya corona ni umaskini unaoongezeka kila siku, na iwapo tatizo la uchumi halitapatiwa ufumbuzi, yumkini idadi kubwa ya watu wakahajiri na kuelekea Ulaya.
Siku chache zilizopita Wakala wa Wakimbizi wa Ulaya (EASO) ulitahadharisha kuhusu wimbi jipya la wakimbizi kuelekea katika nchi za Ulaya na kutangaza kuwa: Maambukizi ya virusi vya corona yanaweza kusababisha wimbi kubwa zaidi la wakimbizi kutoka nchi za magharibi mwa Asia na kaskazini mwa Afrika katika siku zijazo kutokana na athari mbaya za maambukizi hayo.