Russia na Ujerumani: Vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran havina maana
Rais wa Russia na Kansela wa Ujerumani wamesisitiza kuwa, vikwazo vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran havina umuhimu wowote.
Vladimir Putin na Angela Merkel walisema hayo jana Jumatano katika mazungumzo yao ya simu ambapo wameeleza bayana kuwa, hatua ya Marekani ya kutumia mashinikizo ya vikwazo dhidi ya Iran haijazaa matunda yoyote.
Idara ya Habari ya Ikulu ya Russia (Kremlin) imemnukuu Rais Vladmir Putin akisema katika mazungumzo hayo ya simu na Merkel kuwa, kuna haja ya kubakishwa kama yalivyo makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, na kama yalivyoidhinishwa na Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Wawili hao wameeleza bayana kuwa, sera ya Washington ya kutumia mashinikizo na vikwazo haijafua dafu na kwamba pande zote husika zinapaswa kufungamana na mapatano hayo ya nyuklia ya Iran.
Haya yanajiri wakati huu ambapo Marekani imekuwa ikifanya jitihada na kutumia visingizio visivyo na msingi kwa lengo la kuzuia kuondolewa vikwazo vya silaha dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa mujibu wa Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Vikwazo hivyo vya silaha dhidi ya Iran vinatazamiwa kuondolewa ifikapo tarehe 18 mwezi Oktoba mwaka huu.