Borrell: Mapatano ya Trump hayawezekani, JCPOA ilindwe
Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya kwa mara nyingine tena amesisitizia udharura wa kulindwa na kuheshimiwa makubaliano ya nyuklia ya Iran yanayofahamika kwa kifupi kama JCPOA, na kueleza bayana kuwa ni jambo lisiloyumkinika kufikiwa kile kinachoitwa "Mapatano ya Tump."
Josep Borrell amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa: Tunapaswa kuyalinda mapatano ya Iran, na nitaendelea kutekeleza wajibu wangu kama mshirikishi wa Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA.
Amesema anaamini kuwa makubaliano hayo yanapaswa kudumishwa kwa sababu mbili kuu: Mosi, hatuna chaguo jingine au mbadala wa mapatano hayo kwa sasa, na Pili, dhana kwamba tunaweza kuunda makubaliano mengine, kwa jina la 'Mapatano ya Trump' ni jambo lisilowezekana.
Mkuu wa Sera za Nje wa EU ameongeza kuwa, ilichukua miaka 12 kufikia mapatano haya, na huo ukawa ushindi mkubwa katika uga wa dipomasia na kuzingatiwa maamuzi ya pande kadhaa.
Borrell amebainisha kuwa, hakuna utawala wowote ukiwemo wa Washington, unaoweza kuweka mezani mapatano bora na athirifu mbadala wa JCPOA.
Hii ni katika hali ambayo, licha ya nchi za Ulaya kudai kuwa zinataka makubaliano hayo yaendelee kulindwa kutokana na mchango wake muhimu katika kulinda usalama na amani ya kikanda na kimataifa, lakini zimekataa kutekeleza ahadi zao zinazofungamana na mapatano hayo, hususan utekelezaji wa mfumo maalumu wa mabadilishano ya kifedha na kibiashara na Iran maarufu kama INSTEX, kutokana na mashinikizo ya Marekani na ukosefu wa azma na irada ya kutosha.