Sisistizo la Borrell kuhusu kulindwa JCPOA; nara isiyotekelezeka kivitendo
(last modified Mon, 20 Jul 2020 06:47:06 GMT )
Jul 20, 2020 06:47 UTC
  • Sisistizo la Borrell kuhusu kulindwa JCPOA; nara isiyotekelezeka kivitendo

Umoja wa Ulaya (EU) na Troika ya Ulaya inayoundwa na Ujerumani, Ufaransa na Ujerumani ni pande zilizokuwa na nafasi muhimu katika kufikiwa mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).

Lakini baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano hayo EU na Troika ya Ulaya  zimekuwa na utendaji mbovu katika kulinda mapatano hayo na utekelezaji wa ahadi zao hasa kuhusu kuanzishwa mfumo wa kifedha wa INSTEX. Lakini pamoja na hayo, Umoja wa Ulaya unasisitiza kuhusu kulindwa JCPOA. Kuhusiana na nukta hiyo, Josep Borrell Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya siku ya Jumamosi alituma ujumbe kupitia Twitter na kusisitiza kuhusu umuhimu wa kulindwa JCPOA. Borrell ameashiria umuhimu wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA katika kikao cha Mazungumzo ya Mediterranean (2020 MED) na kusema: "Katika mwaka wa tano wa kufikiwa mapatano ya JCPOA, nilizungumza kuhusu mapatano hayo katika Kikao cha Mazungumzo ya Mediterranean Mwaka 2020." Josep Borrell amebainisha zaidi kuhusu maudhui hiyo kwa kusema: "Sisi tutayalinda mapatano ya JCPOA na mimi nitaendelea na shughuli zangu kama mratibu wa Tume ya Pamoja ya JCPOA."

Rais Donald Trump wa Marekani mnamo Mei 8 2018 alitangaza uamuzi wa upande mmoja wa kukiuka azimio 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA ya mwaka 2015 yaliyofikiwa baina ya Iran na madola ya kundi la 5+1 pamoja na Umoja wa Ulaya. Baaada ya uamuzi huo uliokiuka sheria za kimataifa, Trump alianzisha mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran ili kuishinikiza Tehran isalimu amri na kutekeleza matakwa yaliyo kinyume cha sheria ya Washington.

Mapatano ya JCPOA

Nchi za Ulaya ziliahidi kuchukua hatua za kushirikiana kwa ajili ya kukabiliana na athari hasi za vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran. Moja ya ahadi hizo ilikuwa ni kuanzisha mfumo maalumu wa kifedha baina ya nchi za Ulaya na Iran unaojulikana kama INSTEX ambao haungeathiriwa na vikwazo vya Marekani. Lakini baada ya kupita miaka miwili mfumo wa INSTEX haujatekelezwa kivitendo na Ulaya. Inavyoelekea ni kuwa nchi za Ulaya zimeshinikizwa na Marekani na pia hazina irada inayohitajika ya kutekeleza majukumu yao ya JCPOA hasa mfumo wa INSTEX.

Kwa msingi huo kuna shaka kuhusu madai ya Borrell kuwa Umoja wa Ulaya unalipa umuhimu suala la kulindwa JCPOA kwa ajili ya kulinda usalama na amani kieneo na kimataifa. Ni wazi kuwa  matamshi ya Umoja wa Ulaya na Troika ya Ulaya kuhusu JCPOA ni nara tupu.

Uchunguzi kuhusu hatua zilizochukuliwa na Umoja wa Ulaya baada ya Marekani kujiondoa katika JCPOA unaonyesha kuwa, umoja huo ni dhaifu na hauna uwezo wa kutekeleza ahadi zake kwa Iran.

Troika ya Ulaya imekataa kutekeleza ahadi zake katika JCPOA kwa kisingizio cha Iran kuchukua hatua za kisheria za kupunguza utekelezaji wa ahadi zake katika JCPOA. Hii ni katika hali ambayo Iran imepunguza utekelezwaji wa ahadi zake katika JCPOA kama jibu kwa nchi za Ulaya kutotekeleza ahadi zao katika mapatano hayo. Kufuatia hatua hiyo ya Iran, nchi za Ulaya zimeanzisha mchakato wa kutatua hitilafu katika JCPOA kwa lengo kutaka kurejesha faili la nyuklia la Iran katika Baraza la Usalama.

Josep Borrell Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya ambaye pia ni mratibu wa JCPOA alitangaza Ijumaa kuwa, kwa kuzingatia kuwepo janga la COVID-19 na ugumu wa kufanyika mkutano wa ana kwa ana wa kuchunguza hitilafu katika JCPOA ambao umeitishwa na Iran, muhula wa utatuzi wa mgogoro uliopo umeongezwa.

Kwa kuzingatia misimamo inayokinzana  ya nchi za Ulaya kuhusu JCPOA, na sisitizo la kulinda mapatano hayo kwa upande mmoja na kwa upande wa pili nchi hizo kushindwa kutekeleza majukumu na ahadi zao, ni wazi kuwa kuna ushirikiano wa karibu baina ya Ulaya na Marekani katika sera za mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran. Lengo la ushirikiano wa pande hizo mbili za Atlantiki ni kushinikiza Iran ili isiwe na budi ila kutekeleza matakwa 12 ya Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ambayo aliyatangaza mwaka 2018.

Iran imetahadharisha kuwa, ilikubali kutekeleza JCPOA katika fremu ya maslahi yake ya kitaifa. Kama alivyosema Sayyed Abbas Mousavi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran: Tehran inazitaka nchi tatu za Ulaya zifungamane na ahadi zilizotoa katika kulinda na kutekeleza kikamilifu JCPOA badala ya kuchukua mkondo wa mashinikizo ya juu zaidi ya Marekani.

Ni bora Umoja wa Ulaya na Troika ya Ulaya kuacha kutoa matamshi na madai ya kuunga mkono JCPOA pamoja na ahadi tupu na iwapo kweli zinataka kulinda JCPOA zichukue hatua za kivitendo na ziache kuandamana na Marekani katika hatua zake dhidi ya Iran.

Tags