Russia yaapa kilipiza kisasi vikwazo vya Umoja wa Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i62541-russia_yaapa_kilipiza_kisasi_vikwazo_vya_umoja_wa_ulaya
Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetangaza kuwa nchi hiyo itajibu mapigo ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya shirika la ujasusi la Russia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 31, 2020 22:48 UTC
  • Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova
    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetangaza kuwa nchi hiyo itajibu mapigo ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya shirika la ujasusi la Russia.

Alkhamisi iliyopita Umoja wa Ulaya uliiwekea vikwazo Russia kwa kisingizio cha kufanya mashambulizi ya mtandaoni. 

Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Ulaya ilisema kuwa, vikwazo vipya vya umoja huo vinalenga kitengo cha teknolojia makhsusi cha shirika la ujasusi la jeshi la Russia.

Taarifa ya umoja huo imeongeza kuwa, kitengo cha teknolojia makhsusi cha jeshi la Russia kimefanya mashambulizi manne ya mtandaoni dhidi ya nchi ya Ukraine na vilevile dhidi ya Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali huko The Hague nchini Uholanzi katika miaka ya 2015, 2016, 2017 na 2018.

Russia imekadhibisha madai ya kuhusika na mashambulizi hayo.

Umoja wa Ulaya umekuwa ukiwawekea vikwazo wanasiasa, wasomi na mashirika mbalimbali ya Russia kwa kutumia visingizio tofauti.