Harris: Sera za Trump dhidi ya Iran zimeifanya Marekani itengwe zaidi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i63068-harris_sera_za_trump_dhidi_ya_iran_zimeifanya_marekani_itengwe_zaidi
Makamu wa Joe Biden, mgombea wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa rais wa mwezi Novemba mwaka huu nchini Marekani amesema sera za Rais Donald Trump dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimeifanya nchi hiyo itengwe zaidi wakati huu kuliko wakati wowote ule.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 27, 2020 21:53 UTC
  • Harris: Sera za Trump dhidi ya Iran zimeifanya Marekani itengwe zaidi

Makamu wa Joe Biden, mgombea wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa rais wa mwezi Novemba mwaka huu nchini Marekani amesema sera za Rais Donald Trump dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimeifanya nchi hiyo itengwe zaidi wakati huu kuliko wakati wowote ule.

Seneta Kamala Harris wa jimbo la California nchini Marekani ambaye hivi karibuni alikubalia kuwa mgombea mwenza wa Biden katika uchaguzi mkuu ujao nchini Marekani amesema misimamo ya utawala wa Trump dhidi ya Iran imelifanya taifa hilo libakie pweke.

Mwanasiasa huyo ameeleza bayana kuwa: Nipo katika Kamati ya Intelijensia, na naamini kuwa hivi sasa tumetengwa zaidi na waitifaki wetu, tunahitaji msaada wa kuondokana na changamoto hii.

Amesema iwapo chama chake kitashinda katika uchaguzi ujao wa urais, basi serikali ijayo itarejea katika mapatano ya kidiplomasia ya nyuklia na Iran sanjari na kushirikiana na waitifaki wa Washington.

Kamala na Biden

Seneta huyo wa California amesema hivi karibuni Marekani ilidhalilika katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutokana na sera na misimamo ya serikali ya Trump, kiasi cha matakwa yao kukosa uungaji mkono katika baraza hilo.

Siku chache baada ya Marekani kushindwa kufanikisha njama yake ya kurefusha vikwazo vya silaha dhidi ya Iran kupitia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Rais wa kiduru wa taasisi hiyo ametupilia mbali ombi jingine la Washington la kutaka kutekelezwa utaratibu wa kurejesha vikwazo vya UN dhidi ya Iran unaojulikana kama 'Snapback Mechanism'.