China yaonya: Ikilazimu, tutaingia katika makabiliano ya kijeshi na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i63108-china_yaonya_ikilazimu_tutaingia_katika_makabiliano_ya_kijeshi_na_marekani
Jeshi la China limetahadharisha kuwa, huenda litalazimika kuingia katika makabiliano ya kijeshi na Marekani pasi na kukusudia iwapo Washington haitasitisha operesheni zake za kichokozi katika Bahari ya Kusini ya China.
(last modified 2026-04-29T03:42:39+00:00 )
Aug 29, 2020 19:31 UTC
  • China yaonya: Ikilazimu, tutaingia katika makabiliano ya kijeshi na Marekani

Jeshi la China limetahadharisha kuwa, huenda litalazimika kuingia katika makabiliano ya kijeshi na Marekani pasi na kukusudia iwapo Washington haitasitisha operesheni zake za kichokozi katika Bahari ya Kusini ya China.

Msemaji wa Jeshi la Ukombozi wa Watu wa China, Kanali Li Huamin amesema, "tunaiomba Marekani isitishe mienendo yake ya kichochezi na ichunge harakati zake za baharini ili kuepusha uwezekano wa kutokea 'ajali' za kijeshi."

Amekosoa vikali kitendo cha manowari ya jeshi la Marekani kuingia kinyume cha sheria na pasi na idhini katika maji ya China.

Msemaji wa Jeshi la Ukombozi wa Watu wa China ameeleza bayana kuwa, Marekani inakiuka sheria za kimataifa za ubaharia na kwa kiburi inaendelea kuchochea taharuki katika Bahari ya Kusini ya China kwa kisingizio cha 'uhuru wa ubaharia.'

Hivi karibuni China ilifyatua makombora ya balestiki katika Bahari ya Kusini ya nchi hiyo kuionya US 

Serikali ya Beijing sanjari na kubainisha kukasirishwa kwake na hatua hiyo na kuitaka Marekani isitishe vitendo vya uchochezi katika Bahari ya Kusini ya China, imesisitiza kuwa ina mamlaka kamili ya kujitawala katika eneo hilo ambalo lina utajiri mkubwa wa maliasili.

Hii si mara ya kwanza kwa Jeshi la Majini la Marekani kupeleka meli zake za kivita karibu na visiwa vilivyoko katika Bahari ya Kusini ya China, mbali na kufanya luteka za kijeshi mara kwa mara katika maji hayo ya China.