Russia na China zapongeza kikao cha Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA
Russia na China zimepongeza mkutano wa Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA uliofanyika jana Jumanne huko Vienna, mji mkuu wa Austria.
Ofisi ya Ubalozi wa Kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa imesema katika taarifa kuwa: Mkutano uliozaa matunda wa Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA katika kipindi hiki nyeti. Washiriki wote wamesisitiza juu ya kulindwa na kutekelezwa kikamilifu makubaliano hayo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, "Ni imani ya pamoja kuwa Marekani haiwezi kuanzisha mchakato wa kutekelezwa utaratibu wa kurejesha upya vikwazo ilivyokuwa imewekewa Iran huko nyuma na UN unaofahamika kama 'Snapback Mechanism."
Wakati huohuo, Mwakilishi wa Russia katika taasisi za kimataifa zenye makao yao mjini Vienna Austria amesema, kwa kauli moja, nchi zilizosalia katika makubaliano ya nyuklia ya Iran ya JCPOA zimetangaza kuwa haziitambui Marekani kuwa mwanachama au mshirika wa mapatano hayo ya kimataifa.
Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, Mikhail Ulyanov amesema: Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA imethibitisha leo (jana Jumanne) kwa sauti moja kuwa Marekani si mshiriki wa makubaliano hayo ya nyuklia, kwa kuwa ilijiondoa kwayo Mei 8 mwaka 2018.
Taarifa ya kamisheni hiyo inayoongozwa na Helga Schmid, Naibu Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya imesisitizia udharura wa kuendelea kuheshimiwa na kutekelezwa makubaliano hayo kama yalivyopasishwa katika Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka 2015. Kadhalika Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA imesema Marekani haina haki ya kutumia utaratibu wa 'Snapback Mechanism" wa kurejesha upya vikwazo ilivyokuwa imewekewa Iran huko nyuma na UN.