Save the Children yaikosoa Ulaya kwa kuwapuuza watoto wadogo wakimbizi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i63180-save_the_children_yaikosoa_ulaya_kwa_kuwapuuza_watoto_wadogo_wakimbizi
Shirika la Save the Children limezikosoa nchi za Ulaya kutokana na zinavyowapuuza watoto wadogo wakimbizi.
(last modified 2025-11-20T09:10:15+00:00 )
Sep 02, 2020 14:58 UTC
  • Save the Children yaikosoa Ulaya kwa kuwapuuza watoto wadogo wakimbizi

Shirika la Save the Children limezikosoa nchi za Ulaya kutokana na zinavyowapuuza watoto wadogo wakimbizi.

Anita Bay Bundegaard, Mkurugenzi wa shirika hilo la Okoa Watoto barani Ulaya ameashiria jinsi watoto wengi wanavyoishia kwenye mipaka ya kuingilia nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya huku wakipoteza maisha katika mazingira hayo; na akakosoa vikali upuuzaji na kutojali kunakoonyeshwa na viongozi wa nchi za Ulaya kwa suala hilo.

Bi Bundegaard amezungumzia kifo cha Alan Kurdi, mtoto mdogo mkimbizi wa Kisyria ambaye alifariki mwaka 2015 baada ya kuzama katika maji ya Bahari ya Mediterania na akakumbusha kuwa, baada ya kifo cha mtoto huyo, viongozi wa nchi za Ulaya walikuwa wa mwanzo kutoa kauli kwamba, tukio kama hilo halipasi kutokea tena, lakini baada ya kupita miaka mitano tangu lilipojiri tukio hilo watoto wadogo wangali wanazidi kukumbwa na hatari wakati wanapohajiri kuelekea Ulaya.

Kitoto Alan Kurdi kilichoaga dunia baada ya kughariki baharini

Mkurugenzi wa shirika la Okoa Watoto barani Ulaya amebainisha kuwa, watoto wanaendelea kufa kwenye mipaka ya kuingilia Ulaya huku viongozi wa nchi za Ulaya wakiwa wanatazama tu hali hiyo kwa mbali.

Katika muda wa miaka mitano iliyopita watoto wasiopungua 70 wamefariki dunia wakati wakivuka Bahari ya Mediterania kwa ajili ya kuelekea barani Ulaya.

Mgogoro wa wakimbizi ambao haujawahi kushuhudiwa, uliozitanza nchi za Ulaya, ni matokeo ya siasa za Magharibi za kuingilia masuala ya mataifa mengine hususan ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.../