Makabiliano ya Marekani na China Mashariki mwa Asia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i63238-makabiliano_ya_marekani_na_china_mashariki_mwa_asia
Waziri wa Mambo ya Nje wa China amewatolea wito wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) kuendelea kupinga uingiliaji wa Marekani katika eneo hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 05, 2020 06:38 UTC
  • Makabiliano ya Marekani na China Mashariki mwa Asia

Waziri wa Mambo ya Nje wa China amewatolea wito wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) kuendelea kupinga uingiliaji wa Marekani katika eneo hilo.

Akizungumza mkutanoni huko Beijing, Wang Yi amepongeza  mazungumzo ya nchi wanachama wa jumuiya ya ASEAN na jitihada zinazofanywa na nchi hizo kupinga uingiliaji wa Marekani katika masuala ya kanda hiyo. 

Hapa kunajitoleza swali kwamba, wito wa China kwa nchi wanachama wa jumuiya ya ASEAN ikizitaka ziendeleze upinzani wao dhidi ya uingiliaji kati wa Marekani katika kanda hiyo una lengo gani? Wito huo una umuhimu katika pande kadhaa. Mosi, ni kuwa China imetoa wito huo katika hali ambayo mivutano katika uhusiano wa Beijing na Washington imefikia kileleni  kutokana na siasa za Washington  za kuingilia masuala ya mashariki mwa Asia. 

Wawakilishi wa  nchi wanachama wa Jumuiya ya ASEAN

Nukta ya pili ni kuwa, China inahitilafiana na baadhi ya nchi jirani kuhusiana na masuala kadhaa zikiwemo hitiliafu zao katika Bahari ya Kusini mwa China. Japokuwa hitilafu hizo ni za muda mrefu lakini katika miaka ya karibuni zimeongezeka na kushadidi zaidi. Wachina wanaona kuwa Marekani inatumia fursa hiyo kuingilia masuala ya eneo hilo. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Wang Yi Waziri wa Mambo ya Nje wa China akasema kuwa, baadhi ya nchi za kigeni zinaibua hitilafu katika Bahari ya Kusini mwa China kwa maslahi yao ya kijio-politiki kwa lengo la kuvuruga na kumwamisha mawasiliano baina ya nchi jirani. 

Nukta ya tatu ni kuwa, siasa za kistratejia za Marekani mashariki mwa Asia katika miaka ya karibuni zimejikita zaidi katika kuanzisha muungano wa kukabiliana au kuisambaratisha China. Kwa mfano tu, Marekani inatumia vibaya hitilafu zilizopo juu ya umiliki wa visiwa na maeneo ya baharini katika Bahari ya Kusini mwa China kama kisingizio cha kuasisi kambi za kiusalama na miungano ya kieneo.  

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani Mike Pompeo hivi karibuni alisema kuhusu suala hilo kwamba: "Leo hii tunapanua siasa za Marekani katika eneo kubwa linalosumbuliwa na hitilafu katika Bahari ya Kusini mwa China. Dunia haitairuhusu Beijing itumie Bahari ya Kusini kama himaya yake ya baharini." Jambo lililo wazi ni kuwa, matamshi haya  ya viongozi wa Marekani yanaonyesha namna Washington ilivyojielekeza zaidi katika sera za kukabiliana na China. 

Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani  

Weledi wa mambo wanaitaja Bahari ya Kusini mwa China kuwa ni eneo ambalo huwenda likawa uwanja wa mzozo mkubwa wa kijeshi katika siku zijazo. Weledi hao wa mambo wanasisitiza kwamba, katika mazingira ya sasa kila moja kati ya China na Marekani inataka kulidhibiti eneo hilo kwa njia tofauti.  

Katika upande mwingine katika fremu ya siasa zake za kuondoa hali ya mivutano, China inafanya juhudi za kuzungumza na nchi jirani ili kuzipatia ufumbuzi hitilafu za mipaka kwa njia ya amani. Kinyume chake, Marekani inaibua hali ya mivutano katika eneohilo na kuingilia masuala ya ndani ya China lengo likiwa ni kuzusha hitilafu zaidi mashariki mwa Asia na eti kuizingira China. 

Marekani imezidisha juhudi za kuisambaratisha China katika hali ambayo hii leo nchi hiyo si tu mzalishaji wa vifaa vidogo vya michezo vya bei nafuu, bali ni mzalishaji mkubwa zaidi wa bidhaa mbalimbali muhimu duniani na inazalisha bidhaa hizo mara tatu zaidi ya Marekani. Seikali ya Marekani inasumbuliwa na nakisi ya bajeti ya dola bilioni 700 katika sekta ya uzalishaji wa bidhaa, ilhali China ina ziada ya bajeti ya dola bilioni 230. Nchi hiyo karibu kila mwezi huzalisha tani milioni 60 za chuma, nembo ya uchumi wa kisasa, na inaipita Japan mara saba katika uwanja huo na kuwa nchi ya pili duniani.  

Kiujumla tunapasa kusema kuwa, mahusiano ya kisiasa na kiuchumi ya dunia ya sasa yanaonyesha kuwa nchi wanachama wa jumuiya ya ASEAN licha ya kuhitilifiana na Beijing katika masuala ya kisheria, zimeandaa uwanja wa kuboresha mahusiano katika nyanja mbalimbali na nchi ya China. 

Sambamba na uhakika huo, eneo la mashariki mwa Asia hivi sasa linashuhudia makabilianao ya pande mbili yanayotofautiana kikamilifu; yaani hatua za kuibua mivutano za Marekani na zile za kuondoa mivutano za China. Pamoja na hayo viongozi wa China hawajanyamaza kimya kuhusu stratejia hiyo ya kuzusha mivutano ya Marekani na wanaamini kwamba, suala hilo ni mstari mwekundu kwa serikali ya Beijing.