Taiwan; mstari mwekundu wa China
Ijumaa ya jana tarehe 18 Septemba, jeshi la China lilianza kufanya luteka ya kijeshi jirani na Taiwan katika kipindi hiki cha anga ya mzozo na mvutano baina ya Beijing na Taipei.
Hata hivyo swali la msingi ni kuwa, lengo hasa la China la kufanya maneva haya ya kijeshi ni nini? Kwa nini katika wiki za hivi karibuni mvitano baina ya Taipei na Beijing umeshadidi? Na katika anga hii je safari za viongozi na maafisa wa Marekani huko Taiwan zimekuwa na taathira katika kushadidisha mvutano huu?
Manuva ya kijeshi ya China jirani na Taiwan yameanza katika hali ambayo, Jumatatu iliyopita, Marekani ilianza kufanya maonyesho ya kijeshi ya siku 12 kando kando ya Kisiwa cha Guam iliyoyapa jina la Valiant Shield. Katika mazingira hayo, Taiwan nayo kwa sasa inafanya maonyesho ya michezo ya computer ya vita yaliyopewa jina la Han Kuang.
Katika uchambuzi wake kuhusiana na malengo ya maonyesho hayo ya kijeshi, gazeti la Taiwan la Liberty limeandika: Maonyesho ya michezo ya computer ya vita yaliyopewa jina la Han Kuang, ambayo yanahesabiwa kuwa ni mazoezi ya ushabibishaji ya computer, yanafanyika kwa lengo la kukabiliana na tishio la China.
Tukiachilia mbali shughuli za kijeshi za Marekani katika eneo, katika majuma ya hivi karibuni safari za kwenda na kurudi za viongozi na maafisa wa Marekani huko Taiwan nazo zimeongezeka sana. Hivi sasa Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani katika masuala ya Ustawi wa Uchumi, Nishati na Mazingira yuko katika mji mkuu wa Taiwan Taipei ambapo jana alitarajiwa kukutana na kufanya mazunguzmo mjini Taipei na Tsai Ying Wen, Kiongozi wa Taiwan.
Kile ambacho kiko wazi ni kuwa, uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Taiwan, unapingana kikamilifu na misingi ya taarifa ya pamoja za mwaka 1972, 1978 na 1982 zilizotiwa saini. Hati hizo za makubaliano kimsingi zinapinga harakati yoyote ile ya kutaka kujitenga Taiwan na China.
Vyovyote itakavyokuwa, kile ambacho kiko wazi na bayana ni kuwa, China itaitambua Taiwan kama sehemu ya ardhi yake; na harakati za Marekani pamoja na hatua ya Washington ya kuiuzia silaha Taiwan inakiuka mamlaka ya kujitawala Beijing. Kwa maneno mengine ni kuwa, Taiwan inahesabiwa kuwa mstari mwekundu wa China na Beijing haiwezi kuvumilia uingiliaji wa aina yoyote ile wa mataifa mengine ikiwemo Marekani katika masuala yake ya ndani.
Sun Jong, mtaalamu wa masuala ya kijeshi wa China aliyeko mjini Beijing anasema kuwa kuwa: Monyesho ya kijeshi siyo tu kwamba, yanabeba ujumbe wa indhari kwa Taiwan inayotaka kujitenga na kwa uingiliaji mambo wa Marekani, bali unaongeza uwezo na nguvu za kivita za China.
Kiujumla tunapaswa kusema kuwa, kufanyika maonyesho ya kijeshi ya China sambamba na yale ya Marekani na Taiwan, ni ishara ya wazi ya kuongezeka mvutano katika Bahari ya Kusini mwa China na Bahari ya Pacific na kushadidi hatari ya kutokea makabiliano. Hata hivyo kuna swali linabakia nalo ni kwamba kwa nini Marekani katika miezi ya hivi karibuni imeshadidisha mno mashinikizo yake dhidi ya serikali ya Beijing?
Inaonekana kuwa, jibu la swali hili linapaswa kuchunguzwa katika tathmini na uchambuzi wa gazeti la Le Monde la Ufaransa. Alan Ferchon, mwandishi na mchambuzi wa gazeti la Le Monde anaamini kuwa, China hii leo imegeuka na kuwa mshindani muhimu wa Marekani na inakwenda sambamba na Marekani katika mambo mengi na katika mustakabali itakuwa nchi na dola lenye nguvu zaidi duniani; hii kwa hakika ndio sababu kuu ya vuta nikuvute inayoshuhdiwa baina ya Washington na Beijing.