Sep 30, 2020 12:35 UTC
  • Azerbaijan yadai imeua maelfu ya askari wa Armenia, UN yatoa kauli

Azerbaijan inadai kuwa imeua maelfu ya wanajeshi wa Armenia katika mapigano yanayoendelea kushuhudiwa katika mpaka wa nchi mbili hizo tokea siku ya Jumapili.

Shirika la habari la Anadolu la Uturuki limenukuu taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Azerbaijan inayosema kuwa, wanajeshi 2,300 wa Armenia wameangamizwa katika mapigano hayo ya kugombania eneo lenye utata la Nagorno-Karabakh.

Vyombo vya habari vya nchi mbili hizo jirani vinasema kuwa, makumi ya watu wakiwemo maafisa usalama na raia wameuawa, huku mapigano hayo yakiingia siku yake ya nne leo Jumatano.

Huku hayo yakijiri, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa taarifa likizitaka nchi mbili hizo zilizokuwa za Umoja wa Kisovieti zisitishe mapigano hayo mara moja.

Taarifa hiyo iliyopasishwa na nchi zote 15 wanachama wa Baraza la Usalama kadhalika imeunga mkono mwito uliotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres wa kuzitaka pande mbili hizo zichukue hatua za kupunguza taharuki baina yao, sanjari na kurejea katika meza ya mazungumzo yenye manufaa. 

Eneo linalozozaniwa la Nagorno-Karabakh 

Kabla ya hapo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupitia Waziri wa Mambo ya Nje Muhammad Javad Zarif ilisisitiza kuwa, kuna haja kwa nchi mbili hizo jirani kutochukua hatua zitakazoendelea kuwasha moto wa vita na taharuki; na kuziasa serikali za Yerevan na Baku kuanzisha mazungumzo haraka iwezekanavyo, katika fremu ya sheria za kimataifa.

Tangu mwaka 1991, nchi hizo mbili zimekuwa zikipigania jimbo la Nagorno-Karabakh lililojitangazia uhuru wake baada ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti. Eneo hilo liko katika ardhi ya Azerbaijan lakini linaedeshwa na watu wa makabila ya Armenia.

 

 

Tags