Iran: Kuanzisha uhusiano na Israel kunaupa hisia ya kinga utawala huo
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva amelaani hatua ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel na kusisitiza kuwa, mienendo hiyo haitakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuufanya utawala huo wa Kizayuni ujihisi umepata kinga zaidi ya kutowajibishwa.
Esmaeil Baghaei Hamaneh amesema hayo katika hotuba yake mbele ya kikao cha 45 cha Baraza la Haki za Binadamu la UN jana Jumatano na kuongeza kuwa, kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo ghasibu mbali na kuufanya uwe na kiburi zaidi, lakini pia utapelekea kufutwa kabisa haki za msingi na zisizopingika za taifa madhulumu la Palestina.
Ameeleza bayana kuwa, hali ya Palestina ni moja ya migogoro ya haki za binadamu ya muda mrefu zaidi duniani tangu uasisiwe Umoja wa Mataifa miaka 75 iliyopita, na kwamba hali hiyo inazidi kuwa mbaya siku hadi siku.
Mwandiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Iran amebainisha kuwa, utawala huo unaotumia mbinu za kigaidi hivi sasa umegeuka na kuwa utawala wa kibaguzi wenye kutumia nguvu za kijeshi.
Amesema utawala haramu wa Israel hauoni haya kujiarifisha kama utawala ambao uwepo wake umejengeka katika misingi ya falsafa ya ubaguzi wa rangi na ubaguzi wa kimatabaka.
Katika hotuba yake hiyo, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva amenukuu matamshi yaliyowahi kutolewa na mwanaharakati wa amani na mpinga ubaguzi wa Afrika Kusini, Desmond Tutu ambaye alisema, 'miamala ya Israel kwa Wapalestina inanikumbusha na inashabihiana na mfumo wa kipindi cha utawala wa ubaguzi wa rangi (apartheid) nchini Afrika Kusini, bali hata zaidi.'