Onyo kali la China la kuzitungua ndege za kivita za Marekani
Kufuatia kushadidi mivutano na mikwaruzano kati ya China na Marekani, Beijing imeonya kuwa ikiwa ndege zisizo na rubani, ndege za kivita au vyombo vingine vyovyote vya kijeshi vya Marekani vitashambulia ardhi au visiwa vya China na kuisababishia hasara, hapana shaka vitalengwa na kutunguliwa.
Indhari ya China ya kuzilenga ndege za kivita za Marekani inatolewa wakati Washington ingali inaendeleza sera zake za uingiliaji wa kikanda kwa kuingilia masuala ya ndani na ya maeneo yanayoizunguka China.
Kwa maneno mengine ni kwamba, licha ya indhari na maonyo yanayotolewa na China, Marekani ingali inaendelea kuunga mkono mpango wa Taiwan na maeneo mengine wa kujitenga na China, ambapo katika miezi ya karibuni safari za maafisa wa Washington kuelekea Taiwan zimeongezeka zaidi.
Kama vile haitoshi, ndege za ujasusi za Marekani zinaendelea kuranda kwenye anga ya Bahari ya Kusini. Hatua zote hizo za Marekani katika eneo la mashariki ya Asia zinaendelea kuchukuliwa, wakati hivi karibuni gazeti la habari za kijeshi la Marekani la Stars and Stripes lilitoa ripoti inayoonyesha kuwa Washington inaweza ikaamua kutumia uwezo wa ndege zake zisizo na rubani za droni aina ya MQ-9 katika maeneo kama Bahari ya Kusini ya China.
Lakini zaidi ya hayo, kuna picha kadhaa zilizochapishwa na vyombo vya habari vya Marekani likiwemo jarida la jeshi la wanamaji la nchi hiyo zinazoonyesha mazoezi ya kijeshi ya jeshi hilo na utumizi wa aina hiyo ya ndege zisizo na rubani za MQ-9 zikilenga adui bandia wa kivita, ambaye kupitia vivuli vya rangi nyekundu vya taswira yake, inaonekana adui huyo ni China. Lakini pamoja na yote hayo, suali la msingi linaloulizwa ni, jeshi la Marekani linafuatilia malengo gani katka eneo kupitia utumiaji wa ndege hizo zisizo na rubani?
Kwa mtazamo wa vyombo vya habari vya China, kazi maalumu ziliyopewa droni za MQ-9 katika eneo kama la Bahari ya Kusini ni kuhamasisha fikra za waliowengi katika eneo hilo dhidi ya China. Gazeti la Global Times limeandika yafuatayo katika kuzungumzia nukta hiyo: "Jeshi la Marekani linatumia droni kwa ajili ya uchochezi wa kidhahania na utengezaji wa taswira na picha za kubuni za vita vya China na Marekani; na inavyoonyesha hiyo ni harakati ya kuchochea na kuhamasisha fikra za waliowengi."
Jambo lililowazi ni kuwa, mara kadhaa China imekosoa rasmi hatua za kichochezi za Marekani katika Langobahari la Taiwan na Bahari ya Kusini ikizielezea kuwa ni hatarishi; na hata jeshi la China limetoa onyo pia kuhusiana na hatua hizo za Washington.
Kwa mtazamo wa wataalamu, chokochoko zinazofanywa na Marekani katika eneo la mashariki ya Asia zimezidisha hatari ya kutokea mapigano ya kijeshi kati ya nchi hiyo na China. Fukiya Nasha, mtaalamu wa masuala ya kijeshi nchini China anasema: Kutumia Marekani uwezo wa droni aina ya MQ-9 katika mahali kama Bahari ya Kusini ya China ni sawa na kutangaza vita. Akifafanua zaidi Nasha anasema:
"Ikiwa Marekani itaanzisha mashambulio ya aina hiyo, huko kutakuwa ni kutangaza vita na kutakuwa na matokeo mabaya sana kwa Marekani. Hapana shaka kuwa China itaanzisha mashambulio pia ya kujibu mapigo na hasa kwa kuwa katika mazingira haya ndege zisizo na rubani za MQ-9 zitakuwa mlengwa wa operesheni; na jeshi la China lina mbinu nyingi za kukabiliana nazo."

Kwa ujumla inapasa tuseme kuwa, hatua za Marekani za kutuma maafisa wake rasmi huko Taiwan, kuongeza kiwango cha uuzaji silaha kwa kisiwa hicho, kuwepo manowari na meli za Marekani katika Langobahari la Taiwan na vilevile mirando inayofanywa na ndege za ujasusi za Marekani katika anga ya Bahari ya Kusini, vyote hivyo vimezidisha hatari ya kutokea mapigano ya kijeshi kati ya nchi hiyo na China. Bila shaka viongozi wa Marekani wanaelewa vyema wamba, hata kwa mtazamo wa kuudogesha uwezo wake wa kijeshi wa Beijing, China ni dola la tatu lenye nguvu kubwa zaidi kijeshi duniani. Kwa hiyo chokochoko zozote zitakazofanywa na Marekani katika eneo, sambamba na harakati za kutaka kujitenga Taiwan zinazoungwa mkono na Washington vinaweza kuandamwa na moto wa ghadhabu za China, tena basi katika mazingira ambayo Trump hivi sasa anahaha kutafuta mafanikio yoyote yale yatakayoweza kumsaidia katika uchaguzi wa urais wa Marekani unaomkabili.../