Kremlin yakadhibisha madai mapya ya Navalny, yasema anashirikiana na CIA
https://parstoday.ir/sw/news/world-i63761-kremlin_yakadhibisha_madai_mapya_ya_navalny_yasema_anashirikiana_na_cia
Msemaji wa Ikulu ya Rais wa Russia (Kremlin) amekadhibisha tuhuma mpya zilizotolewa na mkosoaji na mpinzani wa serikali ya nchi hiyo na kutangaza kuwa Moscow ina ushahidi unaothibitisha kuwa, Alexei Navalny anashirikiana na shirika la ujasusi la Marekani CIA.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 01, 2020 21:09 UTC
  • Kremlin yakadhibisha madai mapya ya Navalny, yasema anashirikiana na CIA

Msemaji wa Ikulu ya Rais wa Russia (Kremlin) amekadhibisha tuhuma mpya zilizotolewa na mkosoaji na mpinzani wa serikali ya nchi hiyo na kutangaza kuwa Moscow ina ushahidi unaothibitisha kuwa, Alexei Navalny anashirikiana na shirika la ujasusi la Marekani CIA.

Dmitry Peskov amesema kuwa, mashirika ya ujasusi ya nchi za Magharibi yanashirikiana na mkosoaji wa serikali ya Russia, Alexei Navalny. Peskov ameongeza kuwa, hii si mara ya kwanza kwa mpinzani huyo kutekeleza maagizo ya shirika la ujasusi la Marekani CIA.

Kuhusu tuhuma mpya zilizotolewa na Alexei Navalny dhidi ya Rais Vladimir Putin, Msemaji wa Kremlin amesema: Tuhuma hizo hazina msingi wowote, hazikubaliki na ni za kudhalilisha.

Jana Alkhamisi Alexei Navalny alidai kuwa Rais Vladimir Putin wa Russia ndiye aliyeamuru mpinzani huyo apewe sumu. Navalny hakutoa ushahidi wa aina yoyote wa madai hayo. 

Alexey Navalny alipatwa na matatizo ya kiafya tarehe 20 mwezi uliopita wa Agosti akiwa kwenye ndege iliyokuwa ikielekea Moscow kutoka mji wa Tomsk huko Siberia na akalazwa hospitalini. Baadaye alipelekwa Ujerumani kwa ombi la serikali ya nchi hiyo.

Navalny akiongoza maandamano dhidi ya serikali ya Russia, Moscow

Taarifa rasmi iliyotolewa na serikali ya Ujerumani lidai kuwa Alexey Navalny alipewa sumu hatari ya Novichok kwa nia ya kumuua na imeitaka Russia itoe maelezo kuhusu kadhia hiyo. Russia imekanusha vikali madai hayo.

Mpinzani wa serikali ya Russia, Alexey Navalny daima amekuwa akiungwa mkono na Umoja wa Ulaya na Marekani na ana nafasi kubwa katika maandamano yanayofanyika katika miaka ya karibuni dhidi ya serikali ya Russia.