Trump: Israel iendeleze ujenzi wa vitongoji Palestina
Donald Trump, mwanasiasa wa chama cha Republican anayewania kuteuliwa kugombea urais nchini Marekani kupitia chama hicho ameutaka utawala haramu wa Israel uendeleze ujenzi haramu wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Trump ameliambia gazeti la Uingereza la Daily Mail kuwa, ujenzi huo wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina na haswa katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan haufai kusimama hata kidogo. Trump ambaye amekuwa akitoa matamshi ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu katika kampeni zake amedai kuwa: "Ujenzi huo unafaa kuendelea kwa kuwa Wapalestina wanaendelea kufyatua makombora ndani ya utawala haramu wa Israel."
Walowezi wa Kizayuni zaidi ya nusu milioni wanaishi katika majengo 230 yaliyojengwa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu tangu mwaka 1967. Licha ya makelele na ukosoaji wa jamii ya kimataifa, utawala ghasibu wa Israel umekuwa ukiendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kzayuni katika ardhi za Wapalestina kinyume cha sheria za kimataifa.
Viongozi wa nchi kadhaa zikiwemo Uingereza, Canada, Ufaransa na Mexico, wamejitokeza hadharani kukosoa misimamo ya chuki na kibaguzi ya Donald Trump.