Russia: Marekani ndio mvunjaji mkubwa zaidi wa haki za binadamu duniani
Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswisi amesema Marekani ndio mkiukaji mkubwa zaidi wa haki za binadamu duniani.
Gennady Gatilov amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kusisitiza kuwa, nchi inayoongoza kwa kukanyaga haki za binadamu duniani ni Marekani. Ameitaka Washington kushughulikia ukiukaji wa haki za binadamu unaoshuhudiwa nchini humo badala ya kuzituhumu nchi nyingine kuwa wakiukaji wa haki hizo.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Russia ameeleza bayana kuwa: Marekani inapaswa kuyashughulikia matatizo ya ndani ya nchi hiyo badala ya kuzielekezea nchi nyingine kidole cha lawama na tuhuma.
Ujumbe huo wa Twitter wa Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswisi ni radiamali kwa ujumbe wa Twitter wa Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ambaye jana alikosoa hatua ya kuidhinishwa Russia, China na Cuba kujiunga na Baraza la Haki za Binadamu la UN.
Gatilov amesema Pompeo amefumbia macho faili jeusi la ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na Washington ndani na nje ya Marekani, na kwamba madai kuwa inaheshimu haki za binadamu ni bwabwaja tu.
Siku ya Jumanne, Russia, China na Cuba na nchi nyingine 12 zilipigiwa kura kujiunga na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, huku Saudi Arabia ikipiga mweleka katika jitihada zake za kujiunga na taasisi hiyo ya UN.