EU yaikosoa Israel kwa kuendelea kupora ardhi za Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/world-i64048-eu_yaikosoa_israel_kwa_kuendelea_kupora_ardhi_za_wapalestina
Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amekosoa uamuzi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 16, 2020 04:12 UTC
  • EU yaikosoa Israel kwa kuendelea kupora ardhi za Wapalestina

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amekosoa uamuzi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Katika taarifa jana Alkhamisi, Josep Borrell ameitaja hatua hiyo ya Israel ya kujenga maelfu ya nyumba za walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina unazoendelea kupora huko Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na katika maeneo ya mji wa Quds kuwa kinyume cha sheria na ni uchukuaji wa maamuzi ya upande mmoja.

Borrell amesema kuendeleza ujenzi huo haramu wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi kunaweka katika hatari ya kutoweka utambulisho wa maeneo ya Wapalestina, na kufifiliza matumaini ya kuundwa taifa huru wa Palestina kwa kufuata vigezo vya kimataifa vilivyokubalika.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya amekariri msimamo wa EU wa kutotambua mabadiliko yoyote yasiyozingatia Mipaka ya 1967 katika ardhi hizo za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.

Jumapili ya Oktoba 4, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu alitangaza kuwa, utawala huo wa Kizayuni utaanza kujenga nyumba 5,400 za Wazayuni kwenye ardhi za Wapalestina karibuni hivi, wiki chache baada ya nchi mbili za Kiarabu za Imarati na Bahrain kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala huo pandikizi.

Nyumba za walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina

Tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2020, utawala wa Kizayuni umeshavunja nyumba 506 za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi huku nyumba 134 zikiwa ni za Wapalestina wa Quds Mashariki.

Kwa mujibu wa azimio nambari 2334 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ujenzi wa vitongoj vya walowezi wa Kizayuni ni kinyume cha sheria.