Hali si shwari Marekani, Mbunge wa Democrat amvaa Pompeo
Mkuu wa Kamati ya Masuala ya Kigeni ya Bunge la Marekani amemlaumu vikali waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, Mike Pompeo, kutokana na majigambo yake kuhusu kukabidhiwa madaraka kwa serikali ijayo ambayo Pompeo ametamba kwamba itakuwa ni ya Donald Trump.
Mtandao wa habari wa Hill umemnukuu Eliot Engel, mbunge wa chama cha Democratic wa jimbo la New York ambaye pia ni Mkuu wa Kamati ya Masuala ya Kigeni ya Bunge la Marekani akisema: Pompeo anazidi kuchochea madai ya uongo ya Donald Trump ya kuweko udanganyifu mkubwa wa kura katika uchaguzi wa Marekani.
Amesema, inashangaza kumuona Pompeo anafanya mashambulizi hatari na yasiyo na msingi na kuuweka chini ya alama ya kujiuliza mfumo mzima wa uchaguzi nchini Marekani.
Aidha amesema, kwa kweli viongozi wote wa Marekani wanapaswa kuachana na madai yao ya kutokea udanganyifu katika uchaguzi wa Novemba 3, nchini humo. Aidha amesema inabidi kura zote zihesabiwe.

Siku ya Jumanne, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo alizungumza na waandishi wa habari na kujigamba kwamba zoezi la kukabidhi madaraka litafanyika nchii humo, lakini si kwenda kwa serikali ya Joe Biden, bali kwa serikali ya awamu ya pili ya Donald Trump.
Donald Trump na wenzake kama Mike Pompeo wameanza kufuatilia mahakamani madai yao ya kuweko udanganyifu mkubwa katika uchaguzi wa rais nchi humo. Wamechukua hatua hiyo katika hali ambayo vyombo vingi vya nchi hiyo, hata televisheni zinazomuunga mkono kwa hali na mali Donald Trump kama vile Fox News zimetangaza kuwa, Joe Biden ndiye aliyeshinda urais katika uchaguzi wa Novemba 3, 2020 huko Marekani.